Video ya mchungaji mmoja nchini akimuombea kijana mmoja ili kupata nguvu za kiume imewagawanya wanamitandao katika makundi mawili kinzani.
Katika video hiyo ambayo mtumishi huyo wa Mungu anayejiita nabii Jeremiah Kioko, aliipakia kwenye ukurasa wake wa TikTok akimuombea jamaa mmoja ambaye alisema ana majini ya kummaliza nguvu.
Nabii Kioko anaonekana akianza kumuombea kijana huyo ambaye amesimama na ghafla anaanza kutetema kama kichaa na kubidi watu waliokuwa wanamzunguka kumshika kwa nguvu hadi kumuinua juu.
Mchungaji anazidisha maombi ya kukemea majini yamwachilie kijana wa watu na hata kwa wakati mmoja anaonekana akimzaba kofi kichwani kijana huyo kama njia moja ya kufukuza pepo la jini.
Jamaa huyo baada ya kukaa kama anazimia anawekwa chini kwenye sakafu na baada ya dakika za kuhesabu nabii anamuamrisha kusimama. Kijana anasema kuwa awali alikuwa anahisi kuumwa na mbavu lakini baada ya toba alidokeza kujihisi mzima na hata kudhihirisha hilo kwa kurukaruka.
Kijana huyo ndio anazidi mbele na kusema kwamba ana ombi lingine la kutaka nabii Kioko kumwombea nguvu za kiume ambazo alisema ni tatizo kwake kwa muda mrefu.
Baada ya kusimama, nabii anamuuliza jinsi anavyohisi naye anajibu kwamba hatimaye nguvu za kiume ni kama zimerudi na anahisi kabisa amejaa.
Nabii huyo anamwambia kuitizama kamera moja kwa moja na kumpa mkewe ujumbe ambaye anamtazama kutoka nyumbani kupitia runinga na kumhakikishia kwamba atarejea nyumbani na kuanzisha vita ya tatu ya dunia baada ya kupokea uponyaji wa nguvu za kiume.
Unaamini maombi ya wachungaji kuombea masuala kama hayo ya kibaolojia ama ni mitikasi tu ya mitandaoni?