Wema Sepetu ajibu madai ya kuwa mjamzito baada ya video akiwa na ujauzito kusambaa

Wema hata hivyo alikuwa na matumaini kwamba siku moja atapata mtoto wake mwenyewe.

Muhtasari
  • Hii ni kwa sababu ya klipu fupi ya video iliyoibuka hivi majuzi, ikimuonyesha malkia huyo akiwa na ujauzito uliokua.

Kupitia kwenye mitandao ya kijamii haswa mtandao wa tiktok habari zimeenea kwamba mwanamitindo na mwigizaji kutoka Tanzania Wema Sepetu kwa sasa ni mjamzito.

Hii ni kwa sababu ya klipu fupi ya video iliyoibuka hivi majuzi, ikimuonyesha malkia huyo akiwa na ujauzito uliokua.

Video hiyo hata hivyo imezua tafrani mtandaoni, huku baadhi ya wanamtandao wakienda mbali zaidi kumpongeza Wema Sepetu na mpenzi wake Whozu kwa habari hizo njema.

Saa chache tu baada ya video hiyo kusambaa, Wema Sepetu amelazimika kuguswa nayo.

Akitumia akaunti yake ya Instagram katika chapisho la hivi punde, mwanamitindo huyo aliweka wazi kuwa habari hizo za ujauzito zilikuwa za uongo kwa sababu video hiyo ilikuwa imetoka kuhaririwa.

Wema Sepetu naye aliweka wazi kuwa kitendo cha muundaji huyo kufanya video hiyo kilimuuma moyoni.

Hii ni kwa sababu aliifanya kwa ajili ya kujifurahisha tu, ilhali kiuhalisia amekuwa akitaka kupata mtoto lakini kwa bahati mbaya hajaweza.

Wema hata hivyo alikuwa na matumaini kwamba siku moja atapata mtoto wake mwenyewe.

Wiki mbili zilizopita Wema Sepetu alitokwa na machozi ya furaha na kuonesha shukrani na faraja yake kwa jumbe nyingi ambazo mashabiki wake walimuandikia kwenye chapisho la picha alizopakia akisherehekea siku ya kuzaliwa na bintiye mpenzi wake Whozu.

Lola, mtoto wa Whozu na Ex wake Tunda alikuwa anasherehekea kufikisha umri wa miaka 2 na Wema alisimama kama mama kwa mtoto huyo kusherehekea pamoja na Whozu.

Wanamitandaoni waliona jambo hilo kuwa la heri na hawakusita kumwandikia Wema jumbe za kumfariji kwa kukosa mtoto kwa muda mrefu, na kwa jinsi alivyoonesha mapenzi yake kwa mtoto huyo bila kumbagua kuwa si wake.

Wema akitoa shukrani zake kwa mashabiki waliomtumia jumbe za faraja, alizidiwa na hisia na kusema kuwa anawaza tu Mungu angezisikia dua zao na kumjibu ombi lake la kupata mtoto, kwani ana uchu sana kumpakata mwanawe siku moja pia.