Harmonize afunguka kwa nini hajafanya mapenzi mwezi mzima

Konde Boy alidokeza kwamba mahusiano yake ya sasa ni ya mbali hivyo kumnyima muda zaidi na mpenzi wake.

Muhtasari

•Katika taarifa yake kwenye Instastori, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alifichua kuwa hayuko na mwanamke yeyote kwa sasa.

•Alibainisha kuwa hatamruhusu tena mwanamke yeyote kuishi katika nyumba yake hadi ahakikishe kuwa ndiye mwanamke anayetaka kuoa.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Staa wa Bongo, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amethibitisha kuwa hajashiriki tendo la ndoa ndani ya mwezi mmoja uliopita.

Katika taarifa yake kwenye Instastori, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alifichua kuwa hayuko na mwanamke yeyote kwa sasa.

Konde Boy aidha alidokeza kwamba mahusiano yake ya sasa ni ya mbali hivyo kumnyima muda zaidi na mpenzi wake.

“Ndio, naweza siku 30 bila kukwichi kwichi! sababu sio na yeyote kwa sasa!! Mapenzi ya mbali,” Harmonize alisema siku ya Jumatano.

Mwimbaji huyo alibainisha kuwa hatamruhusu tena mwanamke yeyote kuishi katika nyumba yake hadi ahakikishe kuwa ndiye mwanamke anayetaka kuoa.

“Hutaona msichana yeyote kwa nyumba yangu hadi awe ndio mwanamke wa maisha yangu. Nitakayemuoa. Mwanamke anayeruhusiwa village ukiachilia mbali familia yangu basi awe mfanya biashara au rafiki yangu tena sio rafiki tu, awe rafiki wa karibu sana (Best Friend For Ever) Na iwe sababu maalum,” alisema.

Wakati huo huo, alifichua kwamba aliamuru mfanyakazi wake wa nyumbani kutupa chochote ambacho kimewahi kuachwa nyuma na mtu yeyote aliyemtembelea nyumbani kwake.

“Konde Village ni nyumba safi!! Kuanzia sasa hakuna chama, hakuna kutembea tembea. Aliyewahi kupita pita, hongera. Kama hujawahi kufika, ndio basi tena,” alisema.

Haya yanajiri takriban wiki mbili baada ya mwanamuziki huyo kuropoka hadharani kuhusu aliyekuwa mpenzi wake, Fridah Kajala Masanja.

Mapema mwezi huu, Konde Boy alitishia kufunguka kuhusu utapeli wa Kajala baada ya kubugia chupa kadhaa za tembo na kulewa.

Siku chache baadaye, mwanamuziki huyo aliandika taarifa ndefu kwenye Instagram ambapo alimshambulia Kajala na kumtaka aache kugombana naye kwenye mitandao ya kijamii na badala yake atafute mwanaume wa kumuoa.

Harmonize alidokeza kuwa haijulikani ni kwa nini mama huyo wa binti mmoja bado hajaolewa licha ya umri wake mkubwa.

“Tafuta bwana mzee mwenzio hata mganga kienyeji aliyezeeka zeheka. Acha kubishana na watoto online na kujitia moyo!! Usikute anajua anaweza kukutana na bang la take me back tena!! Kinachomfanya asiolewe hatukijuwi, kazi ni kumfwata fwata binti tuu!! Ukweli unaujua wewe!!” Harmonize alifoka siku ya Alhamisi asubuhi.

Staa huyo alidai kuwa Kajala amekuwa akifika kwake katika jaribio la kuomba msamaha ila walinzi wamekuwa wakimtimua.

“Kama unahisi sijamove on ni tatizo lako la uzee pia!! Sikukugombeza, sikukutukana. Nilikudharau na ndio maana umekuwa ukisema ukisema akimzoea mtu anamdharau. Hakuna aliyekuwa akijua hili hata watu wa karibu ndio maana kila mtu alikuwa anadhani nimecheat na sijui amelowa girl lol,”  alimwandikia ex huyo wake.

Konde Boy alimwita mpenziwe huyo wa zamani 'mwizi' na akamweleza bayana kuwa hafikii hata robo ya sifa za mpenzi wake wa sasa.