Mpenzi wa Hamisa Mobetto atamani sana kupata mtoto naye, akiri bado hajafanikiwa kuitwa baba

Kelvin alifichua kuwa atakutana na watoto wa Hamisa, Fantasy Majizzo na Dylan Abdul Naseeb kwa mara ya kwanza.

Muhtasari

•Kelvin alifichua kuwa yeye binafsi hana watoto lakini akadokeza kuwa anasubiri kwa hamu kupata watoto kadaa na Hamisa.

•Alisema ni matumaini yake kumuoa mama huyo wa watoto wawili na kuwa na familia naye katika siku za baadaye.

Hamisa na mpenzi wake Kelvin Sochax.
Image: INSTAGRAM// KEVIN SOCHAX

Mpenzi wa Hamisa Mobetto, Kelvin Sochax kwa sasa yuko nchini Tanzania kwa mara ya kwanza na anatarajiwa kutembelea nyumbani kwa mwanamitindo huyo maarufu.

Kelvin aliwasili katika nchi hiyo jirani usiku wa kuamkia siku ya Jumatatu na mwanasosholaiti huyo alimkaribisha na maua kabla ya wawili hao kuwa na mazungumzo na waandishi wa habari.

Katika mahojiano hayo, raia huyo wa Togo alibainisha kuwa yupo nchini Tanzania kwa ajili ya mpenzi wake Hamisa. Pia alifichua kuwa atakutana na watoto wa mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz, Fantasy Majizzo na Dylan Abdul Naseeb kwa mara ya kwanza.

"Itakuwa mara ya kwanza kukutana nao na siwezi kusubiri. Huwa tunazungumza kupitia simu, kupitia video ya simu. Tutakutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza,” Kelvin alisema.

Kelvin alifichua kuwa yeye binafsi hana watoto lakini akadokeza kuwa anasubiri kwa hamu kupata watoto kadaa na Hamisa.

"Siwezi kusubiri," alisema.

Mwanaume huyo wa Togo alifichua kuwa alikutana na Hamisa katika hafla ya faragha nchini China na akavutiwa naye mara moja.

Alisema ni matumaini yake kumuoa mama huyo wa watoto wawili na kuwa na familia naye katika siku za baadaye.

"Hatujui mpango wa Mungu ni nini lakini natamani twende kila mahali pamoja hadi mwisho," alisema.

Aidha, aliweka wazi kuwa hakuwahi kujua kuwa Hamisa Mobetto ni supastaa enzi hizo walikutana China na alikuja kujua baadaye.

Kelvin pia alithibitisha kuhusu kulipa mahari kwa mama huyo wa watoto wawili na kusema kuwa suala hilo ni kati yake na yeye.

Katika mahojiano hayo, Hamisa alikana kuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na bosi wa lebo ya Konde Music Worldwide, Harmonize.

Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond alibainisha kuwa hakuna chochote kikubwa kati yake na Konde Boy na kubainisha kuwa mwimbaji huyo wa kibao ‘Single Again’ ni rafiki yake tu.

“Yeye ni rafiki tu. Hakuna zaidi, hakuna kidogo, "alisema.

Baada ya kubainishiwa kuwa Harmonize anayapenda sana makalio yake makubwa, mama huyo wa watoto wawili alikiri kuwa hafahamu hilo.

Wakati alipoulizwa ikiwa anafahamu urafiki wa Harmonize na mpenzi wake, Kelvin aliweka wazi kuwa hata hamfahamu mwimbaji huyo.

"Simjui, simjui," Kelvin alisema.