"Kesho ukituita harusi nyingine tutakuja!" Bahati amliwaza Akothee baada ya kudokeza hajakuwa sawa

Bahati alimhakikishia Akothee kwamba yuko tayari kumsapoti katika jambo lolote litakalomletea furaha.

Muhtasari

•Bahati alimtaja Akothee kama shujaa na hazina katika tasnia ya muziki nchini Kenya na kumhakikishia upendo wao kwake.

"Kukujulisha tu Ata Kesho Ukituita Harusi ingine Tutakuja Mapeeeemaaa juu Furaha Yako ndio Furaha Yetu," Bahati alisema.

 

Bahati, Diana Marua, Akothee
Image: HISANI

Bosi wa EMB Records Kelvin ‘Bahati’ Kioko amemhakikishia mwimbaji mwenzake Esther Akoth almaarufu Akothee kwamba ataendelea kumpa sapoti yake bila kujali chochote.

Katika taarifa yake ya Jumanne, mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili alimtaja Akothee kama shujaa na hazina katika tasnia ya muziki nchini Kenya na kumhakikishia upendo wao kwake.

Alisema kuwa hakuna maoni yoyote ya umma yanayoweza kufafanua mama huyo wa watoto watano na akadokeza kuwa hajali mambo kumhusu ambayo amekuwa akiona mitandaoni.

“Madam Boss, Mama na Rafiki Yangu @Akotheekenya ..,. Hakuna Maoni ya Umma Yanayoweza Kukufafanua... Wewe ni Shujaa na Hazina katika sekta yetu ya muziki wa Kenya, Tunakupenda,” Bahati alisema kupitia Instagram.

Aliongeza, “Naona Maneno Mingi mtandaoni lakini sijalii na mimi sihitaji Ufafanuzi, ilimradi uwe na furaha ndicho kitu cha muhimu Zaidi!!! Ustawi wako ni muhimu zaidi."

Bahati aliendelea kumhakikishia mwimbaji na mjasiriamali huyo mwenye umri wa miaka 43 kwamba yuko tayari sana kumsapoti katika jambo lolote litakalomletea furaha.

"Kukujulisha tu Ata Kesho Ukituita Harusi ingine Tutakuja Mapeeeemaaa juu Furaha Yako ndio Furaha Yetu," alisema.

Bahati na mke wake Diana Marua ni miongoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria harusi ya Akothee na Denis ‘Omosh’ Shweizer iliyofanyika katika bustani la Windsor Golf Hotel & Country Club jijini Nairobi mnamo Aprili 10, 2023.

Ujumbe wa mwanamuziki huyo kwa Akothee unajiri siku chache tu baada ya mama huyo wa watoto watano kudokeza kwamba mambo hayajakuwa sawa kabisa katika miezi michache iliyopita na kwamba amekuwa akishiriki vipindi maalum na mtaalamu wa masuala ya kisaikolojia.

Katika taarifa yake Jumapili jioni, Akothee alifichua amekuwa akihudhuria vikao vya ushauri maalum na mtaalamu wa kisaikolojia na kujaribu kupona faraghani kwa miezi miwili iliyopita katika juhudi za kurejesha afya yake ya akili.

Alifichua kuwa matatizo yalianza baada ya kupata ukweli na maelezo fulani ya kutisha ambayo yalimfanya aingiwe na hofu na kumfanya aingie kwenye dimbwi  la mawazo.

"Nimetoka eneo hatari sana na nimekuwa nikipona kwa faragha, niko kwenye mwezi wa pili wa therapy kufuatia kiwewe nilichopitia baada ya kujua ukweli na mambo mabaya ambayo yaliniacha nikitetemeka, Zilipita siku bila chakula. na hakuna kulala, nilihoji na kujijibu mwenyewe, imekuwa nzito sana. Siku zingine, usiku ungekuwa siku na kuniacha mimi nikitazama nje ya dirisha nikikadiria  yasiyokuwepo, ningejipata nikitetemeka kwa sababu ambazo siwezi kuelezea, na kumbuka bado nilikuwa na kazi ya kufanya, familia na ufalme wa kulinda. Bado nililazimika kuweka uso mkali na kuwaburudisha mashabiki wangu,” alisema. 

Aliwashukuru wote waliosimama naye wakati wa nyakati ngumu alizopitia na kumsaidia kutembea katika safari ya uponyaji ikiwa ni pamoja na marafiki wake wa karibu, familia na meneja wake Nelly Oaks ambaye amemtaja kama rafikiye mkubwa.

"Nelly Oaks amekuwa akipiga simu haraka, akinipigia bila kukoma na alikuwa akiogopa simu yangu ilipokatika, watoto wangu kisawa sawa hasa wasichana tulihakikisha tunaweka timer ili kuangalia kama niko sawa. Rue alinifuata Ulaya kwa hofu. ya kunipoteza, mtoto alinikalisha hadi nikasimama kwa miguu yangu,” alisema mwimbaji huyo.

Aliongeza, "Nilianza kwa kufuatilia mienendo yangu, niligundua kuwa nilikuwa nikilemewa na hisia mara kwa mara bila sababu, hata mahojiano rahisi tu. Nilikuwa nimekosa utulivu, na sikuweza kuweka kidole juu yake. Sikuwahi kujua kuhusu Unyanyasaji wa Kihisia, hadi nilipoanza matibabu. Nilikuwa katika hali mbaya ya akili iliyonifanya nilipe ksh 50,000 kwa saa kwa kipindi cha saa moja na mtaalamu wa kwanza. Nilikuwa nikitetemeka na kupoteza nguvu, hamu ya kula, usingizi, hofu na hata kupoteza motisha katika kufanya mambo niliyopenda kufanya.”

Kufuatia hilo, amewaomba watu kuendelea kumuunga mkono na kumuombea yeye na familia yake wakati wakiendelea kurekebisha mambo faraghani.