Mwimbaji na mjasiriamali wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee ametangaza kuwa atachukua mapumziko kwa wiki kadhaa zijazo.
Katika taarifa yake ndefu siku ya Jumamosi jioni, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alisema kuwa atakosekana kwenye mitandao yote ya kijamii hadi katikati ya Januari mwaka ujao.
Alisema kuwa matukio ya mwaka wa 2023 yamemfanya achoke sana na hivyo anahitaji kupumzika kwa muda ili kurejesha nguvu.
“WAPENDWA MASHABIKI, natumai ujumbe huu utawapata vyema. Nilitaka kuchukua muda kuungana nanyi na kushiriki habari muhimu. Mwaka uliopita umekuwa safari ya ajabu, iliyojaa hali ya panda-shuka, na ninawashukuru kila mmoja wenu kwa kuwa sehemu yake,” Akothee alisema kupitia Instagram.
Aliongeza, “Hata hivyo, jinsi safari ya maisha inavyozidi kuwa mbaya, ninajikuta nikihisi uchovu na kukosa nguvu. Msongamano wa mara kwa mara umeniacha nikiwa na wakati mchache wa kupumzika na kuongeza nguvu, na nimefikia hatua ambayo ninahitaji kutanguliza ustawi wangu.
"Kwa kuzingatia hili, nimeamua kuchukua muda kidogo na kujiepusha na mitandao yote hadi tarehe 15 Januari 2024. Safari hii itaniruhusu kujiongezea nguvu, kuratibu upya na kujikumbusha. Ni hatua muhimu kuhakikisha kwamba ninaweza kuendelea kutoa yaliyo bora kwangu kwenu nyote.”
Mama huyo wa watoto watano alisema kuwa anatumai kurejea akiwa na nguvu zaidi baada ya mapumziko na kuwashukuru wale wote ambao wamemsapoti kwa mwaka mzima.
"Ninaelewa umuhimu wa kuwepo kikamilifu na kutoa bora zaidi, na sitaki kuathiri ubora wa maudhui na uzoefu ninaoshiriki nanyi.. Ninaamini kwamba mtaheshimu hitaji langu la mapumziko haya, na ninatazamia kuungana nanyi nyote katika mwaka mpya, tukiwa tumeburudishwa na tayari kwa matukio mapya,” alisema.
2023 umekuwa mwaka wa kukumbukwa sana kwa mwimbaji, kwa sababu nzuri na mbaya, ni mwaka ambao amefunga ndoa, akachukua talaka, kuhitimu, kati ya mambo mengine mengi ambayo yametokea katika maisha yake.