Size 8 afunguka kuhusu kutaka talaka, afichua kwa nini alitaka kumuacha DJ Mo

DJ Mo alifichua kwamba mkewe alimfahamisha kuhusu nia yake ya kugura ndoa yao kupitia WhatsApp.

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto wawili alifichua kwamba alikuwa amepoteza matumaini katika ndoa yake kiasi cha kutaka kuivunja.

•Size 8 alisema baada ya kuhudhuria mafiunzo, alikubali kutulia na kutazama iwapo mume wake naye angekuwa tayari kuifanyia kazi ndoa yao.

Image: INSTAGRAM// SIZE 8 REBORN

Mhubiri na mwimbaj mashuhuri wa nyimbo za injili Linet Munyali almaarufu Size 8 amefichua kwamba aliwahi kutaka kugura ndoa yake na mtumbuizaji DJ Mo na hata akatafuta usaidizi wa wakili wa talaka.

Wakati akizungumza katika kipindi cha uhalisia kilichopeperushwa kwenye runinga ya TV 47, mama huyo wa watoto wawili alifichua kwamba alikuwa amepoteza matumaini katika ndoa yake kiasi cha kutaka kuivunja.

“Kilichofanyika, ilifika mahali nikawa sina matumaini, nikawa nimefika hatua ya kutorudi nyuma. Nadhani msongo wa mawazo pia ulianza. Kwa hivyo sikuwa nikifikiria sawa na sikuwa nikiona njia ya kutoka. Ndiyo maana niliamua kumwita wakili wa talaka,” Size 8 alisimulia.

Mwimbaji huyo alifichua kuwa baada ya kumweleza mwanasheria wa talaka kuhusu nia yake ya kuvunja ndoa yake, hata alimwelekeza aanze kutayarisha karatasi rasmi za hatua hiyo. Alisema kuwa alitaka kutenganishwa na mcheza santuri huyo na kuruhusiwa kwenda na watoto wao wawili.

Talaka hiyo hata hivyo haikuendelea baada ya mama huyo wa watoto wawili kuzungumza na mamake DJ Mo na pia kuhudhuria likizo ya mafunzo ambayoilimfanya apate hamu ya kuipa ndoa hiyo nafasi nyingine.

“Tuko karibu sana na mama yake. Aliniambia nimekasirika nisifanye mambo kwa haraka. Kisha mhubiri alikuwa ametaja likizo takriban wiki mbili kabla, ilikuwa imebaki mwezi hadi tarehe ya likizo. Nilisema, nitapatia ndoa yangu nafasi moja ya mwisho,” alisema.

Size 8 alisema baada ya kuhudhuria mafiunzo hayo, alikubali kutulia na kutazama iwapo mume wake naye angekuwa tayari kuifanyia kazi ndoa yao.

Akizungumzia kwa nini alitaka kuacha ndoa yake, mwimbaji huyo alisema kuna mambo mengi yalimfanya atake kumuacha mumewe.

"Nilipoenda huko, nilijifunza kweli. Mimi nilikuwa nataka kuacha Mo kwa sababu ya mingi. Yaani ni kama tulikuwa tunaenda njia pande," alisema.

Kwa upande wake, DJ Mo alikataa kuzungumza mengi kuhusu talaka.

Mcheza santuri huyo alidai kutojua alikosana na mkewe kuhusu nini na akafichua kuwa mama huyo wa watoto wake wawili alimfahamisha kuhusu nia yake ya kugura ndoa yao kupitia mtandao wa WhatsApp.

“Mimi nilimwambia sawa, tutaongea kuhusu hilo,” alisema.

DJ Mo na Size 8 wamekuwa kwenye ndoa kwa zaidi ya muongo mmoja na wana watoto wawili pamoja. Wawili hao walifunga pingu za maisha katika hafla ya siri na ya faragha katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu mnamo Septemba 23, 2013.