Staa wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh hivi majuzi alikumbuka jinsi ambavyo alidhihakiwa na mtu wa karibu kwa kuwa yatima.
Msanii huyo mahiri alikuwa akizungumzia tukio la kusikitisha alilokumbana nalo kwenye mitandao ya kijamii aliposimulia tukio lake kama hilo.
Alifichua jinsi alivyomwomba mtu amsaidie pesa za kulipia ziara ya shule, lakini badala yake mtu huyo akamdhihaki kuwa ni yatima.
"Hii ilinikumbusha kwamba wakati fulani nilimsihi 'mtu fulani' anipe 200Ksh kwa safari ya shule kwenda Nakuru crater na alikuwa kama: Sami unafaa ujue wewe ni yatima hufai kujiwekea maisha ya juu," Samidoh alisimulia kupitia Facebook.
Aliongeza, “Kuna mambo ambayo hata Mwanaume mwenye moyo mzito hawezi kupona kutoka kwayo.😢😭. Baadhi ya Ndugu/Wazazi/Walezi wanaweza kukuua ukiwa hai!!”
Baba huyo wa watoto watano alifunguka baada ya kukutana na kisa cha kusikitisha cha yatima aliyeambiwa akachukue mifupa ya marehemu mamake na kuitumia kama kuni.
"Siku ya jumatatu Jioni nilikuwa napitia akaunti yangu ya tiktok. Kitu cha kufurahisha na cha kusikitisha kilivutia macho yangu ya uvivu: "Ni kauli gani iliyokuua Lakini ulijifanya kuwa uko sawa?..
Mtu alishiriki; ‘Baada ya kifo cha Mama yangu tulikaa na Shangazi yetu (Dada ya baba yangu)Siku moja ikawa hakuna kuni, aliamka na akaniambia nifufue mifupa ya mamangu tupike nayo chai ,,” mwimbaji huyo aliandika kabla ya kusimulia tukio lake.
Marehemu Miriam Wairimu alikuwa mkulima mahiri na mwanamuziki kama mwanawe tu. Aliimba nyimbo za injili.
Aliaga dunia wakati Samidoh akiwa bado katika shule ya upili. Baba yake pia alifariki wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2017.
"Nilizaliwa katika familia ya watoto 6, sisi ni wavulana 6 na mimi ni wa tatu kuzaliwa. Mama alikuwa anaitwa Miriam Wairimu lakini alituacha. Na Mzee alikuwa anaitwa Michael Ndirangu. Alikuwa Afisa wa Polisi wa Utawala (AP). Alifanya kazi Nakuru na Molo na alikufa ile wakati wa mapigano," Samidoh alisema katika mahojiano ya awali.
Pia alifichua kwamba alikuwa akiimba pamoja na mamake kanisani na katika mikutano ya kidini. Alisema kuwa marehemu alichangia sana katika mafanikio yake kwenye tasnia ya muziki wa Kikuyu.