Mwanamuziki na mjasiriamali maarufu wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee amefunguka kuhusu baadhi ya masaibu anayokumbana nayo kama mtu mashuhuri.
Katika chapisho la Jumatatu jioni, mama huyo wa watoto watano alikiri kuhisi upweke hadi kufikia hatua ya kuhamia nyumba za jamaa zake.
"Inakuwa upweke sana kuwa staa. Niamini, wakati fulani namiss kupanda matatu bila kuangaliwa. Imekuwa upweke sana kwamba nilihamia nyumba ya dada-mkwe wangu na nyumba za watoto wangu," Akothee alisema kwenye chapisho la Facebook.
Aliongeza, “Wakati fulani mimi hujiuliza kwa nini nilipe ada au kulea watoto ambao sikuzaa pia. Ikiwa bado unaweza kuona posti zangu, andika tu Amen. Ninahisi uchovu & nimechoka 🙏 SIHITAJI LOLOTE ila KUMBATIWA 🙏."
Katika chapisho lingine, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 aliendelea kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusu shirika lake la hisani, Akothee Foundation.
Alilalamika kuhusu baadhi ya watu ambao hakuwataja majina ambao alidai wanamuumiza kwa kutumia wakfu huo ambao anadai kufadhili peke yake kwa usaidizi wa wasamaria wema.
“AKOTHEE FOUNDATION HAINA WAFADHILI WALA WADHAMINI. INATEGEMEA KABISA BRAND AKOTHEE na Esther Akoth Kokeyo na watu wachache wanaokutakia heri wanaokuja mara moja baada ya nyingine.
Kwa nini watu utumie Wakfu wa Akothee kuniumiza na kujaribu kunidhuru? Kwa nini watu wanatumia Wakfu wa Akothee kama jukwaa kuwasiliana nami, na wakati mambo hayaendi sawa, wao hutumia fursa hiyo kuniumiza?
Kwa nini watu huchukua fursa ya udhaifu wangu? Sikujua kamwe kutoa kunaweza kumfanya mtu ajisikie mtupu. Ninajifunza na kuacha kujifunza. Mungu anipe nguvu ya kuendelea.,” Akothee aliandika.
Aliendelea, “Watoto wangu walimaliza shule miaka iliyopita, na watoto wadogo wanatunzwa vyema Ulaya. Kwa hivyo kwa nini DM yangu imejaa watu wanaohitaji usaidizi, ambao baadaye wanapata hisia za kustahiki? Kwa nini watu wanajifanya kusapoti wakfu, na baadaye kuwa wanyonyaji? Hatuna watoaji; tunao watafuta kiki. Nimekuwa nikipitia hisia nyingi za hivi majuzi na sidhani kama nahitaji hii.”
Aidha, mama huyo wa watoto watano alidokeza kuhusu kuchukua mapumziko kwa muda ambao haujafichuliwa ili kupata afueni.