"Asante kwa kuwa baba aliyepo!" Yvette amsifu Bahati baada ya kujitokeza kusapoti binti yao, Mueni

Mama Mueni alionekana kujawa na bashasha wakati akimtazama binti yake akitumbuiza pamoja na mzazi mwenzake, Bahati.

Muhtasari

•Yvette hakuweza kuficha furaha yake huku akimtazama bintiye akitumbuiza na mzazi mwenzake na alisikika akishangilia

•Bahati alisikika akiwashauri wazazi kuwaacha watoto wao wafuate kile wanachopenda.

amemsifu mzazi mwenzake Bahati
Yvette amemsifu mzazi mwenzake Bahati
Image: INSTAGRAM//

Ilikuwa siku nzuri kwa Mueni Bahati huku wazazi wake wote wawili, mwimbaji Kelvin Bahati na mfanyibiashara Yvette Obura, wakijitokeza kumsapoti wakati wa hafla ya kuonyesha vipaji shuleni mwake.

Siku ya Jumamosi asubuhi, Bahati alichapisha picha yake, bintiye Mueni na mwanawe Majesty Bahati wakiwa wamesimama kwenye uwanja wa shule.

"Ni siku ya talanta ya binti yangu Mueni Bahati shuleni kwa hivyo mimi na Majesty Bahati tulienda kumtazama akicheza," Bahati alisema chini ya picha hiyo.

Katika picha hiyo, watatu hao walionekana kuwa na furaha kwa kushiriki muda pamoja.

Kwa upande mwingine, Yvette Obura, ambaye ni mzazi mwenza wa Bahati aliposti video za binti yao akicheza mbele ya umati wa wazazi, wanafunzi na wageni wengine waliokuwa wamekusanyika shuleni.

Katika mojawapo ya video hizo, msichana huyo wa miaka minane alionekana akiimba wimbo wa babayake, ‘Lala Amka’, pamoja na watoto wengine huku umati ukishangilia. Huku akiendelea kutumbuiza, alienda mpaka alipokuwa amekaa Bahati, akamshika mkono na kumtaka asimame na kutumbuiza naye.

“Pigeni makofi basi.. tusimame basi,” Bahati alisema baada ya kukabidhiwa kipaza sauti na bintiye.

Yvette hakuweza kuficha furaha yake huku akimtazama bintiye akitumbuiza na mzazi mwenzake na alisikika akishangilia

Mfanyibiashara huyo pia alichapisha video nyingine iliyomuonyesha Bahati akitoa hotuba kwa wageni, na chini ya video hiyo, alimsherehekea mzazi mwenzake kwa kuwepo kwa ajili ya binti yao.

"Asante Baba Mueni kwa kuwa baba aliyepo na anayekusudia," Yvette aliandika.

Katika video hiyo, mwimbaji huyo alisikika akikiri jinsi anavyojivunia binti yake.

Pia alisikika akiwashauri wazazi kuwaacha watoto wao wafuate kile wanachopenda.

"Nilihisi kama, siamini kumuona binti yangu akifanya kile anachopenda angali mdogo. Najua nyinyi wazazi mko na jukwaa hilo, watoto wakisoma kidogo, unaacha wafanye ile kitu wanapenda. Mungu awabariki nyote, nimefurahi kusikia,” Bahati alisema.

Mueni ni mtoto wa kwanza wa mwimbaji Bahati ambaye alipata na Yvette Obura takriban miaka minane iliyopita, kabla ya wawili hao kutengana.