"Nimechoka kujifanya!" Harmonize akiri kum'miss mpenzi wake siku chache baada ya kutengana

Konde Boy na Poshy Queen waliripotiwa kwenda njia tofauti wiki moja iliyopita baada ya kuwa na migogoro mikali.

Muhtasari

•Katika taarifa yake, Konde Boy alikiri kwamba anam’miss sana Poshy Queen na akasema amechoka kujifanya.

•“Nimechoka kujifanya. Nakumiss Bombo claa,” Harmonize alisema.

Harmonize na mpenzi wake Poshy Queen
Image: HISANI

Staa wa Bongo, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ni wazi anapata tabu kukabiliana na upweke baada ya kutengana na mpenzi wake Poshy Queen.

Konde Boy na mama huyo wa mtoto mmoja waliripotiwa kwenda njia tofauti wiki moja iliyopita baada ya kuwa na migogoro mikali katika uhusiano wao.

Katika taarifa yake ya hivi majuzi kwenye Snachat, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alikiri kwamba anam’miss sana Poshy Queen na akasema amechoka kujifanya.

“Nimechoka kujifanya. Nakumiss Bombo claa,” Harmonize alisema.

Aliambatanisha taarifa yake na picha ya mrembo huyo na emoji za huzuni kuonyesha hali yake.

Mapema wiki iliyopita, Konde Boy na sosholaiti Poshy Queen waliripotiwa kutokuwa katika hali ya maelewano tena.

Mastaa hao wawili ambao wamekuwa wakichumbiana kwa miezi kadhaa sasa waliripotiwa kuvunja uhusiano wao, huku wote wawili wakipeana vidokezo kwa ku-unfollow kila mmoja kwenye mitandao ya kijamii.

Uchunguzi wa kina kwenye majukwaa yao ya mitandao ya kijamii ya Instagram ulionyesha kuwa hawafuatilianii tena kama hapo awali. Haijabainika ni lini hasa waliacha kufuatana hivi majuzi lakini inaaminika kuwa ni punde baada ya kutofautiana.

Chanzo cha matukio ya hivi majuzi bado hakijajulikana kwa umma lakini kumekuwa na taarifa ambazo hazijaripotiwa kutoka Tanzania kuwa bosi huyo wa Kondegang alichukizwa na mpenzi wake huyo kuonekana kutaniania na mwanaume mwingine, tukio lililosababisha waachane.

“Kuna mwanaume alimmiminia Champagne Poshy wakati Harmonize anacheza muziki kule, wapo bize wanavibe pale. Ile ikaleta maneno, Harmonize hakupenda. Akauliza kwa nini anakumiminia Champagne, au anakutaka wewe kwa nini unamchekea. Harmonize akamwaga ile Champagne, wakakasirika ikatokea maneno ya watoto na kuvutana kidogo, wakachukuana wakaondoka,” alisema ripota wa Millard Ayo TV, Vido Vidox.

Aliongeza, “Za kudaiwa zinasema ndio hapo ikabidi Poshy na Harmonize wakazinguana. Poshy akaenda kwake, Harmonize akabaki kwake. Ilipokuja mitandaoni, wakakuta picha zimefutwa. Kila mmoja amefuta picha za mwingine. Alafu kila mmoja amemuunfollow mwenzie “

Wasanii hao wawili wa Tanzania wamekuwa wakichumbiana kwa takriban miezi minane sasa.

Habari kuhusu uchumba wao ziliibuka mapema mwaka huu, na kusababisha mijadala mingi na msisimko kwenye mitandao ya kijamii.