Siku ya Alhamisi, bosi wa WCB Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz alimvizia mpenzi wake Zuchu kwa simu wakati wa mahojiano ya moja kwa moja kwenye Wasafi Media.
Ikiwa unafikiri kuwa simu ilikuwa kwa ajili ya kumpapasa kwa maneno matamu au kumwambia jambo la kimapenzi, umekosea!
Sababu iliyomfanya staa huyo wa bongo kumpigia simu mpenzi wake ilikuwa ni kumuuliza zilipo funguo za mlango ambao hausemwa wazi nyumbani kwao.
“Samahani, niko kwenye mahojiano nakupigia.. funguo?” Zuchu alisikika akimwambia mpenzi na bosi wake kwenye simu.
Malkia huyo wa muziki mzaliwa wa Zanzibar kisha alionekana akitoka nje ya studio ili pengine kumueleza Diamond mahali funguo zipo.
Zuchu alikuwa ameenda katika studio za Wasafi Media kukutana na msanii wa zamani wa Konde Music Worlwide, Anjella na kumkabidhi gari ambalo alikuwa amemnunulia.
Siku ya Alhamisi, binti huyo wa Khadija Kopa alitimiza ahadi yake kubwa ya kumnunulia gari Anjella, ambayo alimpa hivi majuzi.
Anjella ambaye alikuwa ameeleza matatizo ya kutokuwa na gari hakuweza kuficha furaha yake wakati malkia huyo wa WCB akimzawadia gari jipya aina ya Toyota Crown, kama alivyoahidi. Alizamia kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii kueleza furaha yake na kumshukuru Zuchu kwa ishara nzuri aliyokuwa ameonyesha.
“Napenda nafasi hii kukushukuru dada angu @officialzuchu ulichokifanya ni kikubwa sana tena sana umenipa nguvu ya kuinuka tena na umeipa faraja familia yangu wazazi nilikua napata shida sana kuhusu usafiri huu umeniipa gari nakushukuru sana dada angu,” Anjella aliandika kwenye Instagram.
Mwimbaji huyo mwenye sauti nzuri aliambatanisha taarifa yake na picha zake akipokea gari hilo jipya nyeupe Alhamisi jioni.
”Umenionesha upendo mkubwa sana, Mungu akuzidishie mafanikio zaidi na zaidi. Umenifanya nijihisi mpya katika hii dunia umenifanyia jambo kubwa sana katika kipindi ambacho sikua na tumaini lolote. Dada angu @officialzuchu nakupenda sana nakuombea mungu akupe maisha marefu na mafanikio zaidi❤️,” aliongeza.
Zuchu alitoa ahadi ya kumnunulia gari Anjella alipokuwa amepigiwa simu na Diva The Bawse wakati wa kipindi cha moja kwa moja. Alikuwa nyumbani kwa Diamond Jumatano wakati Diva alipompigia simu ili kuzungumza na Anjella.