‘Aryan’, mwana wa Sanjay Bangar; mchezaji wa zamani wa
kriketi ameelezea athari ambazo kwa
mujibu wake anaisi miezi 11 baada ya kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha jinsia
ya kuwa mwanamke kutoka kwa mwanamume.
Kwenye ukurasa wake wa Instagram kitengo cha
matukio(stories) ‘Aryan’ ambaye alibadilisha jina na kuwa Anaya amesema kuwa
tangu kufanyiwa upasuaji huo, amepata furaha zaidi, anatumia nguvu kidogo na
kupungua kwa hofu ya kutokuwa mkamilifu maarufu kama dysphoria pamoja na mabadiliko ya mwili.
Anaya amesema kuwa licha ya kuafikia hayo yote, bado angali
na mwendo mrefu katika safari yake ya kujihisi kamili ila kila hatua anayopiga
anajihisi akiwa yeye.
“Napoteza nguvu lakini ninapata furaha. Mabadiliko ya mwili, kupungua
kwa dysphoria… bado mwendo ni mrefu lakini kila hatua nahisi nikiwa mimi zaidi.” Aliandika Anaya kwenye Instagram.
‘Aryan’ mwenye umri wa miaka 23 alibadilisha jina baada ya
kufanyiwa upasuaji huo na kujiita Anaya Bangar ikimaanisha kuwa anajitambua
kama jinsia ya kike na wala si ya kiume.
Anaya alifanyiwa tiba ya kubadilishiwa homoni (Hormone
Replacement Therapy, HRT) hivyo basi jinsia yake ikabadilika.
Mnamo tarehe 9 Julai mwaka huu, Anaya alichapisha kwenye
Instagram yake picha mbili moja akiwa ‘Aryan’ na nyingine akiwa Anaya
akisherehekea miezi sita tangu kufanyiwa matibabu ya kubadilisha homoni.
Wakati huo Anaya alieleza kuhusu maamuzi magumu aliyofanya
huku upande mwingine akisherehekea ufanisi alioupata kutokana na maamuzi
aliyoyafanya.
“Kutoka kwa wakati wa huzuni, ukandamizaji na aibu hadi kupata furaha
ya kweli katika mageuzi ambayo yamekuwa ya ajabu. Miezi 6 ya HRT, changamoto
zisizohesabika, maamuzi magumu na vita vya kila siku lakini nimefika hapa
nikiwa na nguvu Zaidi na amani tele.”
Alisema Anaya.
Anaya amekuwa akichapisha picha za mabadiliko ya
mwili wake kila baada ya miezi kadhaa kuonyesha namna mabadiliko yanafanyika.