Rapa
maarufu wa Kenya Brian Omollo almaarufu Khaligraph Jones amejibu kwa kejeli
baada ya kundi la wakosoaji kukejeli jumba la kifahari ambalo alimalizia
kulijenga hivi majuzi.
Katika saa kadhaa zilizopita, wakosoaji kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakikejeli jumba kubwa la kifahari ambalo rapa huyo alijenga huku wengine wakilinganisha na jumba la mall.
Katika majibu yake, Khaligraph alionekana kuwacheka wakosoaji hao huku akibainisha kwamba hayo ndiyo aina ya matatizo aliyoyataka.
"Unaamka unapata unatrend sababu umejenga nyumba kubwa inakaa kama maduka, Mungu anajua haya ndio matatizo niliyokuwa natamani," Khaligraph alisema.
Rapa huyo mahiri amekuwa akitrend haswa kwenye mtandao wa kijamii wa X asubuhi ya Jumatatu kwa sababu ya nyumba yake.
Picha ya Khaligraph na mama yake wakiwa wametulia ndani ya jumba hilo kubwa iliwekwa kwenye mtandao wa X Jumapili jioni kabla ya mwanamtandao mmoja kuihariri na kuifanya kuonekana kama duka.
Wanamtandao wengine wengi walichukua picha iliyohaririwa na kuitumia kufanyia mzaha jumba hilo.
Haya yanajiri miezi michache tu baada ya Khaligraph kukamilisha jumba la kifahari ambalo alianza kujenga miaka michache nyuma.
Rapa huyo alianza kuonyesha nyumba yake inayojengwa mwaka 2022, huku baadhi ya wakosoaji wakimshtumu kwa kujigamba.
"Ninaonyesha mafanikio yangu kwa sababu ni kitu ambacho hakikuonyeshwa navijana ambao walikuwa hapa kabla yetu," Khaligraph Khaligraph alisema wakati huo.
Aliendelea na kuongeza, “Najenga nyumba ili kuwaonyesha wanamuziki wengine kuwa ni vizuri kuwekeza kwani kwa tasnia hii mambo yanaweza kubadilika, lakini ukiwa na sehemu ya kuita nyumbani ambapo hulipi kodi ni salama kwa familia."
Mtunzi huyo wa kibao"Tuma Kitu," aliendelea na kuongeza kuwa hakuwa na shinikizo la kutaka nyumba hiyo iwe kwa wakati fulani au kuwavutia watu.
"Naijenga
kwa kasi yangu kwa sababu sina pesa zote hizo, lakini mimi sijengi nyumba za
ufala, najenga nyumba noma. Ni kubwa yenye vyumba vingi vya kulala.
Najisukuma," alisema mwanamuziki huyo.
Pia alisisitiza kuwa alitaka mafanikio yake yawatie moyo watu na kuwakumbusha kuwa hakuna linaloshindikana mtu akiweka nia yake.