Bosi wa Konde Music Worldwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ameonekana kukanusha madai ya kurudiana tena na aliyekuwa mpenzi wake Frida Kajala Masanja.
Mabango yanayoonyesha hafla iliyoandaliwa kusherehekea kurudiana kwa wawili hao mnamo Disemba 15 yamekuwa yakisambazwa mitandaoni, yakisukumwa na mburudishaji Mwijaku.
Kondeboy hata hivyo ameeleza kuwa hafahamu kuhusu tukio kama hilo, akibainisha kuwa pia ameshangaa tu kama wanamtandao wengine ambao wameona mabango hayo.
“Ni nini hasa kinaendelea!! Napigiwa simu nyingi sana tarehe 15 sijuwi best sijuwi nini,” Harmonize alisema.
Mwimbaji huyo aliendelea kueleza kuwa atamfikia Mwijaku ili kupata ufafanuzi wa kinachoendelea kabla ya kuwapasha mashabiki wake kuhusu hilo.
Hii ni ikiwa ni miaka miwili baada ya staa huyo wa bongo fleva
na Kajala kuachana baada ya kurudiana kwa miezi kadhaa.
Mastaa hao walikuwa wamerudiana mwezi Mei mwaka wa 2022 baada ya kutengana mwaka mmoja kabla. Harmonize alifanya juhudi nyingi kumuomba msamaha Kajala na kumtongoza katika juhudi za kumshawishi akubali kufufua uhusiano wao uliovunjika.
Ingawa hakufichua kilichowatenganisha, aliweka wazi kwamba hakubeba kinyongo chochote dhidi ya mwimbaji huyo.
"Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia, ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu," Kajala alisema wakat huo.
Wakati wa mahojiano na kituo cha redio cha hapa nchini mapema mwaka jana, Kajala alidokeza kuwa alimtema Harmonize kwa sababu ya mazoea.
"Sijui niseme nini. Labda mazoea. Mtu akishakuzoea sana anakuchukulia poa," alisema.
Muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alidokeza kwamba Harmonize bado hakuwa tayari wakati alipoamua kutulia naye kwenye mahusiano na kuwa huenda alihitaji nafasi ya kufanya mambo yake binafsi.
"Yaani mimi hata simlaumu, kwa sababu yeye ni kijana mdogo. Labda alihitaji nafasi, tulikuwa tuko karibu sana.
Yeye mara ya kwanza nahisi labda aliona kama mzaha akisema nataka huyu mtu, nataka niwe naye 24/7. Mnaamka wote mnaenda gym, mnafanya hiki na kile. Labda alikuwa anahitaji nafasi yake afanye vitu vyake," alisema.
Kajala alibainisha kwamba alikubali kurudaina na bosi huyo wa Konde Music Worldwide kwa kuwa bado alikuwa anampenda.