Mwanasiasa na mwanasheria maarufu wa Kenya Karen Njeri Nyamu ameapa kumchukulia hatua za kisheria staa wa bongofleva Diamond Platnumz.
Hii ni baada ya mwimbaji huyo kukosa kutumbuiza katika tamasha la Furaha Festival lililoandaliwa katika uwanja wa Nairobi Polo Club mnamo Desemba 7.
Bosi huyo wa WCB alikuwa miongoni mwa wasanii wakubwa waliotarajiwa kutumbuiza kwenye tamasha hilo lililokuwa na mbwembwe nyingi, lakini alikosa kupanda jukwaani akilalamikia kutokuwa na mpangilio mzuri.
Akizungumza katika kipindi cha moja kwa moja cha hivi majuzi kwenye mtandao wa Facebook, seneta Nyamu alielezea kusikitishwa kwake na Diamond na akawaahidi waandalizi wa hafla hiyo kuwa atawasaidia kurejeshewa pesa zao.
“Willis Raburu, mimi ni wakili, mtu asikudanganye ati Karen Nyamu nini, mimi ni Mwanasheria. Nitakusaidia kupata pesa ya Diamond, Willis Raburu unitafute nikuonyeshe vile tutafanyia Diamond huyo,” Karen Nyamu alisema.
Mwanasiasa huyo alikosoa hatua ya bosi huyo wa WCB kutofanya shoo akisema kuwa alilipwa pesa nyingi sana kukosa kupanda jukwaani.
“Hawezi kosa kuperform na amelipwa pesa nyingi sana. Karibu shilingi milioni 20 za Kenya. Huo ulikuwa upuuzi kutoka kwa Diamond Platnumz,” alisema.
Nyamu alisema kuwa alifuatilia drama yote iliyowahusisha Diamond na Willy Paul kwenye simu yake kwani alikuwa mgonjwa wakati huo.
Alidai kuwa Diamond alikuwa akishinikiza kutumbuiza kabla ya Willy Paul kwa sababu alihisi shoo ya mwimbaji huyo wa nyimbo za mapenzi wa Kenya ingekuwa nzuri, kutokana na jinsi alivyowekeza pesa nyingi kwenye hilo.
Pia alipuuzilia mbali madai ya staa huyo wa bongo fleva kuwa alikosa kufanya shoo kwa masuala ya ukosefu wa usalama na ukosefu wa mpangilio mzuri.
“Unafikiri Diamond anaweza kutoka
Tanzania ati anakuja kutegemea usalama wetu? Atoke Tanzania akuwe ati sasa
amekuja kutegemea usalama wetu? Umewahi kuona jinsi Diamond hutembea na walinzi
wake?” alisema.
Mapema wiki hii, Diamond alifichua kuwa alilipwa $150,000 (Ksh19.4m) kutumbuiza jijini Nairobi, Kenya mnamo Desemba 7.
Katika taarifa ya video aliyoitoa siku ya Jumanne, akielezea sababu ya kutotumbuiza, mwimbaji huyo alithibitisha kuwa alilipwa mamilioni ya pesa kutumbuiza lakini alichoshwa na jinsi tukio hilo lilivyotokea kuwa na kumfanya asitumbuize jinsi alivyopanga.
“Mimi nimelipwa pale, nimelipwa dola laki moja na hamsini. Nafikiria hiyo ni milioni 400 za Tanzania,” Diamond alisema.
Bosi huyo wa WCB alipuuzilia mbali madai ya kujilazimisha kutumbuiza jukwaani kabla ya wasanii wengine, kama ilivyodaiwa awali na baadhi ya wasanii wa Kenya.
Pia aliweka wazi kwamba hawezi kurejesha pesa alizolipwa.