Mchekeshaji maarufu wa Kenya Oliver Otieno almaarufu YY Comedian ameonekana kuthibitisha kuisha kwa uhusiano wake wa muda mfupi na mrembo Noela Toywa.
Katika mahojiano na SPM Buzz, baba huyo wa binti mmoja alitangaza kuwa tayari ametengana na mpenzi ambaye alitambulisha miezi miwili iliyopita.
YY alibainisha kuwa watu kutengana baada ya kuisha kwa uhusiano ni jambo la kawaida na akathibitisha kuwa yeye na Noela ni mambo ya zamani.
"Si tuliachana bro, tuliachana tu vile watu huachana," YY alisema.
Mchekeshaji huyo pia alibainisha kuwa watu kutengana ni hali tu ya maisha.
Tulipoangalia kurasa zao za mitandao yao ya kijamii, tulibaini kuwa wawili hao tayari wame’unfollow kila mmoja kwenye Instagram baada ya kutengana.
Haya yanajiri takriban miezi miwili baada ya mchekeshaji huyo kumtambulisha Noela kama mpenzi wake mpya baada ya kuthibitisha kutengana na mzazi mwenzake Marya Okoth.
Mapema Novemba, YY Comedian alimpeleka Noela katika safari ya chopa, na akamuandalia date ya chakula cha mchana kabla ya uzinduzi wa ukurasa wake wa Instagram.
Katika video za mtandaoni, wawili hao walionekana wakiburudika huku wakipanda chopper kuelekea kule walikopanga kwa ajili ya uzinduzi wa akaunti ya Instagram.
"Nilimpeleka msichana wangu kwa chakula cha mchana huku nikimtambulisha kwa dunia... Asante kwa urafiki, @noelatoywa," walinukuu video zao.
Wakati wa kutambulisha Noela kwa umma, YY alikiri kwamba Noela alikuwa ameleta furaha nyingi maishani mwake.
"Umeleta furaha nyingi maishani mwangu na ni heshima kuwa na wewe. Ninahisi kama ni wakati sasa wa kukutambulisha kwa ulimwengu wangu. Pia ninataka watu wakujue na kukuelewa, wewe ni nani, unasimamia nini, na unaamini nini," YY Comedian alisema.
"Kwa hiyo kabla hata hujatuambia wewe ni nani nina kitu cha pekee sana kwako hapa. Hii ni hati miliki ya kipande cha ardhi ambacho nimekununulia. Nataka ufanye chochote unachotaka, ukipendakujenga nyumba, au kufanya biashara ni juu yako," alisema.
YY aliendelea kutoa changamoto kwa mpenzi wake kuchagua maeneo ya ndoto ambayo anataka kusafiri na angefanikisha.
YY na Noela walikuwa wamechumbiana kwa muda sasa baada ya mcheshi huyo kumaliza uhusiano wake na baby mamake, Marya Okoth.