Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya amesema kuwa atalazimika kutafuta shilingi milioni moja ili kuandaa sherehe ya kuwasherehekea wanafunzi waliofanya mtihani wa sekondari mwaka jana kutoka eneobunge lake.
Mbunge huyo ameelezea furaha ya wanafunzi kutoka shule kadhaa katika eneo bunge lake kupata alama bora ambazo zitawawezesha kujiunga na vyuo vikuu nchini.
Kwenye ukurasa wake wa Instagram, PK Salasya amehongera shule ya upili ya wasichana ya Shitoto kwa kuwa na matokeo bora ambapo zaidi ya wanafunzi arubaini wamepata alama za moja kwa moja kujiunga na vyuo vikuu mbali mbali nchini kuendeleza masomo yao katika taaluma na nyanja mbali mbali.
Aidha mbunge huyo amejisifu akidai kuwa tangu kuchaguliwa kama mbunge wa Mumias Mashariki, matokeo ya wanafunzi katika mitihani ya kitaifa imeimarika kutokana na uwekezaji kwa maswala ya elimu na uongozi.
Shule ya Shitoto iliandikisha alama ya wastani ya 7.0 Salasya akiisifia kuwa shule ya mashambani.
“Hii shule kabla sijaingia kwenye uongozi ilikuwa na perfoming vibaya sana lakini nilipoingia kwenye uongozi niliomba mabadiliko makubwa shuleni na kwa support yangu na kwa support yangu madam principal amenipa nilichokuwa nakitaka.” Aliandika Salasya kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Mbali na shule ya wasichana ya Shitoto, mbunge Salasya pia
amesifia shule ya sekondari ya Kamashia ambayo kwenye matokeo yake, wanafunzi
141 wamefuzu moja kwa moja kujiunga na vyuo vikuu. Shule hiyo, iko na alama ya
wastani ya 7.565 inayoashiria alama ya B chanya.
Sherehe ambayo mbunge huyo anapanga kufanyika
mwezi wa tatu itawajumuisha watahiniwa wa mwaka huu.