Mwimbaji na mtayarishaji maudhui mashuhuri nchini Kenya Steven Odero almaarufu Stevo Simple Boy amekiri kusalitiwa kimapenzi mara kumi.
Akizungumza katika mahojiano ya hivi majuzi, mwimbaji huyo wa kibao ‘Mafi Mafi Mushkila’ alibainisha kuwa kusalitiwa kulimfanya kuogopa mambo ya mapenzi.
Stevo alidai kuwa ni vigumu sana kupata mpenzi mwaminifu katika kizazi cha sasa akitangaza kuwa kwa sasa hayupo kwenye uhusiano wowote.
“Nime’cheatiwa mara 10. Mambo ya mapenzi nilichorea hadi 2026. Siku hizi hakuna mwaminifu, wacha nibaki single,” Stevo alisema.
Mwimbaji huyo pia alizungumzia jambo la kuumiza zaidi ambalo mwanamke amewahi kumfanyia, akifichua kwamba mwanamke mmoja ambaye tayari alikuwa na uhusiano na mwanamume mwingine aliwahi kumdanganya kuwa anampenda.
"Alinidanganya ananipenda kumbe ako na mtu," alisema.
Stevo alisema kuwa mwanamke kutokuwa mwaminifu ni shida yake mwenyewe kwani hufanya hivyo huku akijua kuwa ana mwanaume anayempenda.
Akizungumzia sifa zinazoonyesha mwanamke anakupenda, mwimbaji huyo alisema, “Mwanzo awe anakupigia simu kila wakati, anakujulia hali, anakuja kwako, anakufulia ama kukupikia alafu anaenda.”
Mwishoni mwa mwaka jana, Stevo alifichua mipango yake ya kufunga ndoa mwaka 2026.
Alisema yuko tayari kuchumbiana kabla ya hapo.
“Nipo mapumzikoni hadi 2026 hakuna mwanamke anayetaka mwanaume aliyefeli, sina mtoto nje ya ndoa, niliamua kupata watoto tu nikioa, utakuwa na shemeji 2026. Kuchumbiana kunaruhusiwa lakini Ninachumbiana tu mnamo 2026,” alisema katka mahojiano na kituo kimoja cha redio.