
KATIKA kesi isiyo ya kawaida, mahakama ya juu nchini Zambia imetoa uamuzi wa kinyonga anayedaiwa kupatiwa mafunzo ya jinsi ya kumroga rais wa taifa hilo, Hachilema Hakainde kupelekwa katika kituo cha kurekebisha tabia.
Kinyonga huyo ni miongoni mwa vitu vingi vya kishirikina vilivyonaswa na washukiwa wawili – waganga wa kienyeji – ambao walikamatwa Desemba 2024 kwa tuhuma za kuroga rais, jarida la Zambain Observer liliripoti.
Washukiwa hao waawili, Leonard Phiri (43) na Jasten Candunde
(42) wanakabiliwa na makosa mawili: Kumiliki hirizi na Kukiri ujuzi wa uchawi.
Akitoa ushahidi wake mbele ya Mahakama ya Lusaka, Ofisa wa
Idara ya Wanyamapori ya Lilayi, Bright Nkhoma, aliiambia mahakama kuwa kinyonga
huyo ni sehemu ya mkusanyo wa hirizi aina ya juju waliokutwa na watuhumiwa hao.
Lakini ilikuwa jukumu la kinyonga katika njama hiyo
iliyodaiwa kuwaacha kila mtu katika chumba cha mahakama akiwa ameshtuka na
kufurahishwa.
Kulingana na afisa huyo wa idara ya wanyamapori, mnyama huyo
alipewa mafunzo ya kubadili rangi kwa njia ambayo "itamchanganya na
kumdhoofisha" Rais.
Kufuatia "kukamatwa" kwake, kinyonga huyo alitumwa
rehab kwa ajili ya kurekebisha tabia.
Wakati Phiri na Candunde wakisubiri hatima yao mahakamani,
kinyonga huyo sasa anasemekana kuzoea maisha, akipokea "huduma" na
pengine kutafakari maisha yake mafupi katika ulimwengu wa siasa na uchawi.
Wakati wa kukamatwa mwaka jana, Msemaji wa polisi, Rae Hamoonga alisema katika taarifa yake kwamba
washukiwa hao wawili, wanadaiwa kukodiwa na Nelson Banda, mdogo wa mbunge mtoro
Jay Banda, ili kumroga rais.
Jay Banda alitoroka kutoka mikononi mwa
polisi Agosti 2024 akikabiliwa na shtaka la wizi wa kupindukia. Mahali alipo
hajulikani.
Washukiwa hao wawili wanakabiliwa na
mashtaka ya kufanya uchawi, kumiliki hirizi na ukatili kwa wanyama.
Msemaji wa polisi alisema washukiwa hao
walifichua kwamba walikubali kupokea malipo kamili ya $7,400.
"Dhamira yao iliyodaiwa ilikuwa
kutumia hirizi kudhuru" Rais Hakainde Hichilema, alisema taarifa ya
polisi, iliyotolewa Ijumaa.
Kesi hiyo inapoendelea, Watu wanabaki wakiuliza: Nani alijua
hata vinyonga wana taaluma katika uchawi?