“Kiwewe bado kipo!” Mr Seed azungumzia afya yake miezi 3 baada ya ajali iliyotishia maisha yake

Mwanamuziki huyo alithibitisha kwamba yuko katika harakati za kupata afueni kikamilifu.

Muhtasari

•Mr Seed mefichua kuwa bado hajapona kabisa, takriban miezi mitatu baada ya kuhusika katika ajali mbaya iliyomsababishia majeraha mwilini.

•Mr Seed pia alitoa taarifa kuhusu jinsi anavyoendelea kisaikolojia na akaeleza kuwa bado anapambana na kiwewe.

Image: INSTAGRAM// MR SEED

Mwimbaji wa nyimbo za injili na za mapenzi Moses Tarus Omondi almaarufu Mr Seed amefichua kuwa bado hajapona kabisa, takriban miezi mitatu baada ya kuhusika katika ajali mbaya iliyomsababishia majeraha mwilini.

Mwishoni mwa mwezi wa Aprili, baba huyo wa watoto wawili alihusika katika ajali ya kutishia maisha kwenye barabara ya Nairobi-Nanyuki wakati alipokuwa akisafiri na baadhi ya marafiki zake kuenda kuona shamba. Ajali hiyo ilimsababishia majeraha mabaya mwilini huku mmoja wa marafiki zake, Ambrose Khan kwa bahati mbaya akiaga dunia kutokana na majeraha yaliyotokana na ajali hiyo.

Wakati akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha Maswali na Majibu kwenye Instagram Jumatatu, Mr Seed alithibitisha kwamba yuko katika harakati za kupata afueni kikamilifu.

“Je, Umepona kabisa?” shabiki mmoja alimuuliza.

Mr Seed alijibu, “Si 100% lakini ninafika huko. Mungu ananilinda.”

Mwimbaji huyo wa kibao ‘Dawa ya Baridi’ pia alipewa jukumu la kutoa taarifa kuhusu jinsi anavyoendelea kisaikolojia na akaeleza kuwa bado anapambana na kiwewe.

Alijibu, "Kiakili, naweza kusema kwamba ninaendelea vizuri sasa, kiwewe bado kipo."

Takriban miezi miwili iliyopita, Mr Seed alichorwa tattoo maalum ya kukumbuka siku ambayo alinusurika kwenye ajali mbaya ya barabarani.

Katika ukurasa wake wa Instagram, msanii huyo tattoo ya tarehe ‘29/4/2023’  iliyochorwa  kwenye mkono wake wa kushoto.

Mr Seed alionyesha video yake akiwa amelala kitandani baada ya kuchorwa tarehe hiyo ambayo ataikumbuka daima.

Mnamo April 29 mwaka huu, msanii huyo wa zamani wa EMB records aliponea kifo chupuchupu baada ya kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani kwenye barabara ya Nairobi-Nanyuki. Ajali hiyo ilichukua uhai wa mmoja wa rafiki yake na mwenzake kazini, mpiga video Ambrose Khan ambaye alizikwa mwezi jana.

Marehemu Ambrose alikuwa kwenye gari moja na Mr Seed, DK Kwenye Beat, mpiga picha mwingine na mfanyabiashara wakati wa ajali.Yeye ndiye mtu pekee aliyekuwa kwa  gari hilo ambaye alipoteza maisha huku wengine wawili waliokuwa kwa gari ambalo waligonga nalo wakifariki dunia pia.

Mwanamuziki huyo aliweza kutumbuiza kwa mara ya kwanza tangu kunusurika katika ajali hiyo mwishoni mwa mwezi Mei. Alikuwa miongoni mwa wasanii ambao walitumbuiza katika Infinity Tavern, mjini Eldoret ila alitumbuiza huku akiwa na mikongojo mikononi kwani viungo vyake bado havikuwa vimepona kikamilifu.

Hata hivyo, kwa bahati nzuri aliweza kutumbuiza vizuri wikendi iliyopita bila mikongojo.