Jambo maalum analofanya mwajiri wa Rosie kuhakikisha anawatendea watoto wao vyema

“Sasa ninaweza kusafiri kwa amani baada ya Rosie kurudi," Mwajiri wa Rosie alisherehekea.

Muhtasari

•Waajiri wa Rosie wameendelea kushiriki video za muungano wake mzuri na familia yao na kuelezea furaha yao juu yake.

•Alifichua kuwa kurejea kwa Rosie kutamwezesha kusafiri duniani kwani ana uhakika watoto wake watakuwa katika mikono salama.

amerejea Lebanon kwa mwajiri wake.
Nanny Rosie amerejea Lebanon kwa mwajiri wake.
Image: HISANI

Mwajiri wa mwanamke wa Kenya aliyevuma Roseline Atieno almaarufu Nanny Rosie ameendelea kusherehekea kurejea kwake nchini Lebanon.

Rosie ambaye amekuwa akiwafanyia kazi wanandoa maarufu wa Lebanon tangu 2021 alikuwa amerudi Kenya mwishoni mwa mwaka jana na alirejea katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati mapema wiki hii, takriban miezi miwili baadaye.

Kufuatia kurejea kwake, waajiri wa Rosie wameendelea kushiriki video za muungano wake mzuri na familia yao na kuelezea furaha yao juu yake.

"Rosie alitimiza ahadi yake na kurudi kwa mapacha ingawa alipata ofa nyingi. Upendo wa kweli utashinda kila wakati," waajiri wa Rosie walisema kupitia mitandao ya kijamii.

Katika video nyingine inayomuonyesha Rosie akiwa amebeba mapacha hao ambao amekuwa akisaidia kulea, mwajiri huyo alidokeza kuhusu sababu maalum inayomfanya mwanamke huyo anayetoka eneo la Bondo, kaunti ya Siaya kuwatendea vyema watoto wake.

"Mtendee kama malkia, atawachukulia watoto wako kama wake. Asante Rosie,” mwajiri alisema.

Pia alifichua kuwa kurejea kwa Rosie sasa kutamwezesha kuendelea kusafiri duniani kwani ana uhakika watoto wake watakuwa katika mikono salama.

“Sasa ninaweza kusafiri kwa amani baada ya Rosie kurudi. Instabul nakuja," alisema.

Rosie ambaye alipata umaarufu mwishoni mwa mwaka jana kufuatia video yenye hisia kali ya yeye akiiga familia ya mwajiri wake alirejea Lebanon Jumatatu baada ya kuwa na familia yake nchini Kenya kwa karibu miezi miwili. Waajiri wake na watoto wao wawili walimkaribisha kwenye uwanja wa ndege ambapo walikuwa na muungano mzuri sana.

Katika mahojiano ya Desemba mwaka jana baada ya kurejea Kenya, Rosie alisema alijisikia vibaya sana kuwaacha wanandoa ambao amewafanyia kazi tangu Oktoba 2021 pamoja na watoto wao wanne ambao alikuwa akiwatunza.

"Ilikuwa wakati wa huzuni zaidi maishani mwangu. Ilijawa na hisia tofauti kwa sababu kwa upande mmoja nilifurahi kuja kukutana na familia yangu na kwa upande mwingine nilikuwa na huzuni kwa sababu nilikuwa naacha watoto ambao nimeishi nao kwa miaka miwili,” Rozzie alisema.

Mwanamke huyo anayetoka Bondo katika Kaunti ya Siaya pia alifunguka kuhusu uhusiano mzuri na muungano thabiti kati yake na watoto wa mwajiri wake.

Alisema alijisikia kukaribishwa sana alipokuwa na familia ya Lebanon kwani wote walimtendea vyema na walithamini kazi nzuri aliyowafanyia.

“Hapo nilijisikia kuwa nyumbani. Tofauti pekee ni mimi nilikuwa nalipwa. Ninawapenda watoto kwa sababu wanathamini kazi yangu na wananipenda kwa hilo. Walikuwa wakinichukulia kama mzazi wao,” alisema.