Hatimaye video ya kibao ''Mtasubiri' ambacho Diamond Platnumz alimshirikisha msanii wake Zuchu ilipakiwa kwenye mtandao wa Youtube usiku wa Jumanne.
Wimbo huo umepata mapokezi mazuri huku ukijizolea watazamaji zaidi ya laki tano chini ya masaa tisa tu.
Kama tu walivyodokeza katika maonyesho yao ya awali wakati wa uzinduzi wa EP, video ya mwisho ya wimbo huo imesheheniwa na mahaba si haba.
Muungano wa mastaa hao wawili wa Bongo katika video hiyo ni wa kupendeza na kutiliwa shaka hasa kutokana na uvumi ambao umekuwa ukisambaa kwa muda kwamba wanachumbiana.
Video hiyo inaanza Zuchu akiwa katika mazingira ya kanisa naye Diamond akiwa amesimama karibu na bwawa kubwa la maji huku akiwa ameshika ua. Wawili hao wanaonekana wakiwa kwenye mazungumzo ya simu.
Hatimaye Zuchu anaungana na bosi huyo wake karibu na bwawa na hapo ndipo huba linaposhamiri.
Wawili hao wanaoshukiwa kuwa wapenzi wanaonekana wakikumbatiana na kutazamana kwa macho ya mahaba.
Katika dakika ya kwanza, sekunde ya 58 Diamond anaonekana kumbusu malkia huyo kutoka Zanzibar.
Video hiyo imeibua maswali zaidi kuhusu uhusiano wa wanamuziki hao wawili ambao wana ufuasi mkubwa kote bara Afrika.
Tazama hapa:-