"Nilijua kuna mwanamke mwingine na nikaolewa," Dadake Diamond Platnumz afunguka kuhusu ndoa yake

Alifahamu mumewe alikuwa na mke mwingine ila hakuwahi kuwa na mtoto naye.

Muhtasari

•Darleen alisema mumewe mfanyibiashara Mtoro Isihaka ndiye aliye katika nafasi ya kueleza jinsi hali ilivyo katika ndoa yao.

•Darleen amedai kuwa hajawahi kukabiliwa na changamoto zozote kama mke mwenza na ni hali ambayo alijiweka akijua.

Queen Darleen na mumewe Isihaka
Queen Darleen na mumewe Isihaka
Image: HISANI

Mwanamuziki Mwanahawa Abdul almaarufu kama Queen Darleen ambaye ni dada ya Diamond Platnumz amesema anachagua kusalia kimya kuhusu hatima ya ndoa yake licha ya uvumi ambao umekuwepo kuwa alitemwa.

Akiwa kwenye mahojiano na Mbengo TV, Darleen alisema mumewe mfanyibiashara Mtoro Isihaka ndiye aliye katika nafasi ya kueleza jinsi hali ilivyo katika ndoa yao.

Dada huyo mkubwa wa Diamond alisema kwamba licha ya kuwa yeye ni mhusika hana  idhini ya kufichua chochote kuhusu ndoa yake.

"Mwanaume ndiye mwenye kauli. Mara nyingi huwa naheshimu yule ambaye anatakiwa kusema. Napenda kufuatilia protocal. Sijapewa ruhusa ya kuzungumza chochote kuhusu ndoa yangu" Darleen alisema.

Ingawa msanii huyo alisusia kutoboa ya ndani kuhusu ndoa yake, alikiri kuwa mume wake huwajibikia mtoto wao.

Darleen pia aliweka wazi kuwa alipokubali ndoa alifahamu kuwa Isihaka tayari alikuwa na mke mwingine ila hakuwahi kuwa na mtoto naye.

"Ingelikuwa hivo nisingeolewa. Nilikuwa najua yupo na nikaolewa, mbona sio sasa" Queen Darleen alisema.

Mnamo mwaka jana uvumi ulitanda kuwa mwanamuziki huyo ametemwa na mumewe baada ya kuwa katika ndoa kwa kipindi kifupi.

Haya yalijiri baada yake kuacha kupakia picha za mfanyibiashara huyo kwenye kurasa zake za kijamii kama ilivyokuwa ada yake.

Darleen amedai kuwa hajawahi kukabiliwa na changamoto zozote kama mke mwenza na ni hali ambayo alijiweka akijua.