Wakenya wanajulikana kuwa watu wenye bidi sana na ambao wanatekeleza mambo yao kwa haraka mno.
Saa chache tu baada ya maneno ya ‘piki pik ponk’ kusambazwa mitandaoni kutokana na matamshi ya wakili Otieno Willis aliyekuwa akizungumza katika mahakama ya upeo jana, akiwakilisha upande wa walalamishi, sasa maneno hayo yamegeuzwa kuwa mradi wa kuuza.
Producer Motif Di Don ametoa wimbo mpya kutoka kwa wimbo maarufu wa Piki Piki Ponki ambao umekuwa ukivuma tangu ulipotamkwa mahakamani na wakili Willis Otieno.
Motif aliwaacha Wakenya wengi wakishangaa jinsi alivyoangusha midundo kwa kutumia neno linalovuma.
Katika video ambayo alishiriki kwenye Instagram, mhandisi huyo wa sauti alitumia sauti ya Otieno katika wimbo wa Piki Piki Ponki.
Katika video hiyo ambayo imewachekesha Wakenya wengi, Motif aliunganisha video inayomuonesha akisikika na wimbo huo wa kuchekesha na wa wakili huyo huku akitamka maneno hayo ndani ya Mahakama ya Juu.
Wakili huyo aligeuza gumzo la kuzungumziwa mitandaoni Jumatano alasiri baada ya kusema maneno hayo ya mchezo akiufananisha na jinsi mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, Wafula Chebukati alivyoongoza shuguli ya uchaguzi.
“Tumepunguza uchaguzi wetu hadi michezo ya utotoni ya binamu yangu ya 'piki pink ponk, paka mielo disco," Otieno alitamka kabla ya kusimamishwa na majaji huku mahakama nzima ikipasuliwa na vicheko visivyozuilika.
Kitendo cha mzalishaji Motif kuachia midundo saa chache tu kimewashangaza wengi na weledi wake kwani ilikuja haraka mno.
Itakumbukwa bidi ya wakenya katika kufanya mambo mtu anaweza dhani walikuwa wamejipanga imekuwa ikiwashangaza wengi.
Wiki kadhaa zilizopita wakati chama cha Roots kilikuwa kikizindua manifesto yao, palisikika sauti ambayo ilikuwa kama kauli mbiu yao ikisema ‘Tingiza miti’, asubuhi yake watu kadhaa walikuwa washachapisha maneno hayo kwenye nguo zao, jambo hili likiwashangaza wengi kuhusu ni muda upi walitumia kuchapisha nguo hizo.