Mwanawe aliyekuwa mwanahabari maarufu Catherine Kasavuli, Martin Kasavuli hatimaye amefunguka kuhusu maswali ambayo yamekuwa yakiulizwa sana kumhusu, haswa tangu mwishoni mwa mwaka jana taarifa za msiba wa mamake zilipogonga vichwa vya habari.
Kupitia ukurasa wake mpya wa Instagram, Martin alishiriki kipindi kifupi cha maswali na majibu ambapo alinyoosha maelezo kuhusu kile alisema kimeulizwa sana kumhusu.
Hata hivyo, Kasavuli alisikitika kwamba wanabogu wengi na baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa vikiandika mambo yao ambayo yako mbali na ukweli halisi.
Alisema kwamba maswali ambayo yamekuwa yakiulizwa kumhusu ni iwapo ameona na kama ana watoto.
“Ni swali ambali limeulizwa sana kama nimeona na kama nina watoto, lakini wanahabari na wanablogu wamekuwa wakiandika mambo yao. Ukweli wangu ni huu – hapana sijaoa lakini nina mtoto mmoja,” Martin Kasavuli alisema.
Marto pia alifunguka kuwa amekuwa akifanya kazi yake nchini Afrika Kusini lakini akadokeza kuwa hivi karibuni anarudi nchini Kenya. Alisema kuwa taaluma yake ni katika mawanda ya uanahabari kama maam yake ambapo anajishughulisha kama mkufunzi wa mtu anayetaka kupeperusha vipindi kwenye runinga, PR pamoja pia na afisa wa kukuza biashara.
Kijana huyo alielezea ni kwa nini yeye hajawahi onekana kwenye runinga kama mama yake na akasema kuwa anapenda maisha yake nyuma ya kamera, japo anapenda sana kufanya kazi na vyombo vya habari lakini mbali na kamera.
Wengi walishangaa maisha yake yamekuaje haswa tangu kifo cha mamake, ikizingatiwa kuwa ni yeye pekee aliyezaliwa bila ndugu na mtu wa karibu pekee aliyejulikana ni mama yake.
Martin alijibu akasema kuwa ana marafiki wa akribu wapatao 12 ambao wamempa msaada mkubwa kipindi hiki ambapo bado msiba wa mama yake ungali mbichi kichwani mwake.
“Kusema kweli nina marafiki takribani 12 ambao ninawatumainia muda wowote. Na wamekuwa wakisimama na mimi muda wote tangu tulipojua kuwa mama yangu anaugua saratani. Kwa hiyo ni hivyo, nina marafiki wazuri na wa kutegemewa kwa msaada. Baadhi yao wamekuwa wakija huku nyumbani kijijini na wamekuwa name kwa mwezi sasa,” Marto alisema.