Msanii wa miziki ya kizazi kipya kutoka Tanzania Mbosso ametangaza kuwa amepata ajali mbaya ya barabarani saa chache zilizopita akiwa nchini Marekani.
Mbosso ambaye wiki hii alianza ziara yake ya muziki nchini Marekani alipakia msururu wa picha na video kwenye instastories zake akionesha gari aina ya Landcruiser Prado ambalo alikuwa analitumiwa likiwa limegongwa vibaya upande wa mbele na pia kukwaruzwa maeneo ya kando.
Kwenye video moja, alionekana akipatiwa matibabu ya huduma ya kwanza na maafisa wa trafiki wa Marekani huku picha nyingine ikionesha gari la kuvuruta magari mabovu likiwa tayari kulivuta gari hilo lililopata ajalai akiwa ndani mwake kuliondoa barabarani.
Mbosso aliwatoa mashabiki wake wasiwasi kwa kuwahakikishia kuwa hakupata kuumia vibaya sana mbali na maumivu kiasi ya baadhi ya sehemu za mwili wake.
“Alhamdulillah sijaumia sana. Ni maumivu tu kwenye mbavu upande wa kulia, bega na uti wa mgongo. Ila niko salama kabisa Alhamdulillah,” Mbosso alidokeza.
Msanii huyo kutoka lebo ya WCB Wasafi ya Diamond Platnumz alianza ziara yake ya kimuziki Marekani mnamo Februari 10 huko jimbo la Arizona, Februari 11 akaenda kule Seattle na Februari 17 anatarajiwa kuenda jimbo la Colorado japo haijulikani kama shoo hiyo itafanyika kutokana na ajali hiyo iliyomkumba Khan.
Taarifa Zaidi kuhusu hali yake ya afya baada ya tukio hilo itatolewa badae na uongozi wake, ila kikubwa mwenyewe kashazungumza kwamba yuko katika hali shwari.