Mwanatiktoker Brian Chira amezua mjadala mkali mitandaoni baada ya kuonesha wazi nia zake za kumtaka mwanamume mwenzake, mwanablogu Andrew Kibe kimapenzi.
Kupitia Tiktok yake, Chira alipakia video akiwa amevaa wigi la kike na kusema kwamba ameshindwa kujizuia kusema kile ambacho moyo wake umekuwa ukitamani kwa muda mrefu.
Chira alisema kwamba ameshindwa kujizuia kila mara anapoona ndevu za mwanablogu Kibe na kumtaka kumtafuta angalau kwa busu.
“Andrew Kibe haki nakutafuta sababu hizo ndevu zako… Mungu wangu, mimi nakutaka Kibe nakutaka wewe. Hebu njoo nibusu hii midomo yangu…” Chira alisema katika video hiyo.
Watu walifurika kwenye video hiyo ya dakika kama 16 hivi na kutoa maoni mbalimbali, baadhi walimkashifu kwa kumtamani mwanamume mwenzake na wengine wakionesha utayarifu wao kwa kusubiri tamko la mwanablogu huyo mwenye utata asiyekosa kujibu mipigo kwa ukali wa aina yake.
“Nani anasubiri jibu la Kibe kama mimi,” Fatuma Mamake alisema.
“Acha nitumie Kibe hii video ndio tusubiri akimpa huyu mijeledi mikali,” mwingine alisema.
Hata hivyo, wengine walihisi mwanatiktoker huyo chipukizi anadandia kwa jina la Kibe ili kutafuta kiki na umaarufu kupitia kwa jina lake.
Chira anaibua madai ya kumtamani Kibe kimapenzi kipindi ambapo Kenya imegubiwa katika mjadala mkali kuhusu uamuzi wa mahakama ya upeo wiki moja iliyopita kuhalalisha mikusanyiko ya wanachama wa LGBTQ.
Mjadala huo umeenea sana kwa wiki moja iliyopita, jambo ambalo limepelekea viongozi mbali mbali kutoa maoni yao, ambayo kwa mara ya kwanza wamekuwa na sauti moja kukashifu uamuzi huo na kusema LGBTQ haina nafasi katika taifa la Kenya.
Ilianza na viongozi wa makanisa kulikashifu na rais Ruto na mwenzake wa upinzani Raila Odinga walitoa maoni sawa wakisema kwamba katiba ya Kenya inatambua msingi wa kifamilia kujengwa kati ya uhusiano wa mwanamke na mwanamume na si vinginevyo.
Ijumaa, serikali ya Urusi kupitia ubalozi wake nchini ilitoa taarifa sawia ya kusimama na Kenya katika hilo ikifichua kwamba ajenda ya LGBTQ inasukumwa kinyemela na mataifa ya Magharibi, madai ambayo hata hivyo balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman alikanusha vikali akisema kwamba Marekani inaheshimu msimamo wa Kenya katika suala la LGBTQ.