Marioo sasa ndiye msanii mwenye albamu iliyofuatiliwa Zaidi kwenye jukwaa la kupakua miziki la Boomplay.
Kulingana na orodha mpya ambayo imetolewa na Charts Tz, albamu ya msanii huyo inayojulikana kama ‘The Kid You Know’ ndio inashikilia nafasi ya kwanza katika orodha ya albamu 10 za wasanii wa Tanzania ambazo zilitolewa kuanzia mapema miaka miwili iliyopita.
Awali, nusu albamu ya nyota wa WCB Wasafi, Diamond Platnumz, FOA ilikuwa imeshikilia kidedea kwa muda mrefu lakini kijana Marioo kwa kasi ya ajabu amempiku msanii huyo anayetajwa kuwa mfalme wa muziki wa kizazi kipya wa Bongo Fleva.
Chini ya mwana mmoja baada ya kuzindua rasmi albamu zao, Marioo anashikilia nafasi ya kwanza akiwa na streams milioni 95.1 kwenye Boomplay, Diamond akiwa ameshuka hadi nafasi ya pili na albamu yake ya FOA ambayo imejinyakulia streams milioni 94.2.
Aidha, Rayvanny, Harmonize na Alikiba wanafunga orodha ya tano bora na albamu zao za hivi karibuni.
Katika orodha hiyo, wasanii Harmonize, Rayvanny na Mbosso wanaonekana Zaidi ya mara moja kwa albamu zao tofauti ambazo waliziachia chini ya miaka miwili iliyopita.
Barnaba Classic, mkongwe wa Bongo Fleva pia alijishikilia nafasi ya na albamu yake ya Love Sounds Different.
Orodha hii inakuja wakati kuna gumzo pevu mitandaoni kuhusu orodha ya wasanii pendwa wa makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris, ambayo ilitolewa siku mbili zilizopita kuangazia safari yake katika mataifa ya Afrika – Ghana, Zambia na Tanzania.
Katika orodha hiyo ambayo sehemu ya wadadisi wameiita ya kimagumashi, wasanii Diamond na Rayvanny hawakuweza kuonekana ,huku kutoka Tanzania, wasanii Harmonize, Alikiba, Zuchu, Mbosso, Jux na Darassa wakiwakilisha katika orodha ya ngoma 25 ambayo zilitajwa kuwa pendwa kwa Harris.