Mwimbaji wa Mugithi DJ Fatxo kupitia wakili wake amemwandikia mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) akitaka matokeo ya uchunguzi wa Kifo cha Jeff Mwathi kufichuliwa.
DJ Fatxo alisema kuwa anataka matokeo ya uchunguzi ndidi ya kifo cha Mwathi ambaye alikuwa rafiki yake na alifariki katika nyumba yake kwa njia tatanishi kuwekwa wazi kwani suala hilo limemchafulia jina kwa Zaidi ya miezi mitatu sasa.
Ikumbukwe Fatxo na wenzake ndio walikuwa wametajwa kama washukiwa wakuu katika kifo cha utata cha Mwathi na baada ya DCI kukamilisha uchunguzi huo, walimkabidhi DPP faili hiyo ili kutathmini kama Fatxo na wenzake wana kesi ya kujibu au ni weupe kama pamba.
“Mteja wetu kiukweli ameathiriwa kwa kiasi kikubwa na shutuma zinazotengenezwa, kutangazwa na kusambazwa kwa wingi kuhusu jinsi marehemu alivyokumbana na kifo kabla ya muda wake na bila ya msingi wowote kwa madai ya kuhusika na uhalifu kwa mteja wetu.”
“Hali imekuwa nyingi sana kwa muda mrefu sana na hivyo kuathiri maisha ya mteja wetu na hustle zake za muziki/burudani. Hivyo ndiye mtu anayeathiriwa zaidi na ucheleweshaji wowote wa maamuzi na ofisi yako nzuri. Ukweli ni kipengele pekee kinachoweza kumuweka huru mteja wetu kwani yeye ni mateka wa dhana na madai hayo," mawakili wa Faxto walijieleza katika barua hiyo kwa sehemu.
Kwa muda mrefu, tangu mwezi Februari, Fatxo amekuwa akijipata katika kuchafuliwa jina mitandaoni baada ya kudaiwa kwamba alihusika kaitka kifo cha Mwathi ambaye alidondoka kutoka orofa ya 10 ambapo Faxto anaishi.
Baadhi walihisi kwamba Mwathi alilawitiwa kabla ya kudondoshwa kutoka ghorofani jambo ambalo lilishurutisha waziri wa usalama wa ndani Kithure Kindiki kuamrisha DCI kuanzisha uchunguzi upya dhidi ya kifo hicho.
Iliwalazimu DCI kufukua mwili wa Mwathi na baada ya uchunguzi wa maiti yake kukamilika na mwanapatholijia mkuu wa serikali Johansen Oduor, ripiti haikutofautiana kwa aina yoyote na ile ya awali iliyofanywa.
Ripiti hiyo ilipelekea uchunguzi kubaini kwamba huenda Mwathi alijirusha mwenyewe na hakutupwa kama ilivyodaiwa, hivyo kuipeleka faili ya kesi kwa DPP kutoa tathmini la mwisho kuhusu hatima ya kesi hiyo.