Sandra Dacha, muigizaji anayejivunia kuwa na usuli wa jamii ya Wajaluo magharibi mwa Kenya amefichua siri kubwa kuhusu ni kwa nini wanawake wengi kutoka jamii hiyo hawapendi kuolewa na wanaume Wajaluo.
Katika mahojiano na Oga Obinna, Dacha alisema kwamba wasichana wengi Wajaluo wanapenda kusikilizwa na kuhusishwa katika kufanya maamuzi kwa nyumba, jambo ambalo wanaume wengi Wajaluo wanaona kama halifai.
Dacha alitaja kama upuuzi, hulka ya wanaume Wajaluo kutaka kufanya maamuzi peke yao pasi na kuwahusisha wanawake wao kama sababu kuu inayowafanya wanawake wao kutaka kutanua mbawa nje Zaidi wanakopewa nafasi ya kuwasilisha maoni yao mezani.
“Wanaume Wajaluo wanapenda upuuzi tu ule wa kutotaka wanawake wafanya maamuzi, wanaona ni kama mwanamke hafai kufanya maamuzi wala hafai kuuliza mwanamume maswali mahali ametoka. Sisi hatuwezi kubali hivyo,” Dacha alisema.
Muigizaji huyo alisema kwamba wanaume wengi huwa hawapendi kutoka na wanawake wao kwenda mitoko ya tafrija na kusema kuwa kama mwanamume ameoa mwanamke na amemweka chini ya miliki yake, basi hafai kuingiwa na kiwewe mkewe anapotaka kutoka naye kwenda popote.
“Kama mimi ni mali yako, na unataka kwenda mahali, mbona usikwende na mimi? Unaniacha kwa nyumba nikifanya nini, si sisi wote ni kitu kimoja? Ndio maana hatupendi upuzi, wanaume Wajaluo hawapendi kuulizwa mahali wametoka,” alisema.
Dacha hata hivyo alisema kwamba wanaume wao wanapendwa na warembo kutoka kabila zingine ambao hawatilii maanani kile ambacho wao – wanawake wajaluo – wanakitilia maanani.
Pia alisema wanawake Waluhya nao ni kama wao kwa kile alisema pia hawapendi wanaume vichwa ngumu kama wanaume Wajaluo.
Kwa utani, Dacha alisema kuwa wanawake Wajaluo pia hawapendi kukaliwa akizua mzaha kwamba yeye anamkalia sana Akuku Danger.
“Wanawake Wajaluo pia hatupendi kukaliwa. Badala yake ni sisi ndio tunakalia. Unaona vile mimi nakalia Akuku, mbaya sana,” alisema.