Diamond avunja kimya baada ya kuingizwa jukwaani wikendi akiwa ndani ya jeneza - video

Kwa kuchora taswira ya haraka, ukumbi huo uliokuwa na taa zenye mwanga wa kudidimia uligeuka na kuwa kama kilinge cha matambiko ya kishirikina.

Muhtasari

• Diamond sasa amevunja kimya kuhusu tukio hilo na kukiri kwamba alipatwa na mchecheto wa aina yake kulala ndani ya jeneza.

Diamond Platnumz ndani ya jeneza.
Diamond Platnumz ndani ya jeneza.
Image: X

Katika tamasha la kampuni ya Wasafi linaloendelea kwenye mikoa mbali mbali nchini Tanzania, wasanii wanaotumbuiza kwenye taamsha hilo wamekuwa wakija kwa ubunivu ainati ilmaradi kuvutia umakini wa mashabiki na kuleta uchachu wa kipekee kila wanapotua jukwaani.

Sasa tukio kubwa ambalo limegonga vichwa vya habari wikendi katika Wasafi Festvial ya wilaya la Raungwa huko Lindi ni lile la msanii kinara wa wasafi Diamond Platnumz kusindikizwa jukwaani akiwa ndani ya jeneza.

Katika tamasha hilo lililofanyika usiku wa kuamkia Jumapili, jukwaa liliandaliwa kwa utofauti mkubwa huku taa za vioo zikiwa zimewashwa na kwenye Kamba kulikuwa kumening’inizwa vitu vilivyoonekana kama mifupa ya binadamu.

Kuingia jukwaani, wanaume wanne waliokuwa wamevalia mavazi ya kujisitiri kabisa walibeba jeneza mabegani na baada ya kuitua chini, kila mtu alibaki kinywa wazi kumuona Simba Diamond akitoka ndani na kunza kutumbuiza.

Kwa kuchora taswira ya haraka, ukumbi huo uliokuwa na taa zenye mwanga wa kudidimia uligeuka na kuwa kama kilinge cha matambiko ya kishirikina.

Diamond sasa amevunja kimya kuhusu tukio hilo na kukiri kwamba alipatwa na mchecheto wa aina yake kulala ndani ya jeneza.

“Kutoka ndani ya jeneza ulikuwa ni uzoefu wenye ukakasi wa kutisha Zaidi kwangu ndani mle,” alikiri.

Hata hivyo, yeye si msanii wa kwanza kuwasili jukwaani akiwa ndani ya jeneza.

Itakumbukwa wasanii mbali mbali akiwemo Ibraah kutoka Konde Music Worldwide aligonga vichwa vya habari wakati mmoja pia baada ya kuingia jukwaani akiwa amebebwa kama maiti.

Nchini Kenya pia msanii rapa Khaligraph Jones aliwahi washangaza wengi na kuvutia maoni kinzani mwaka 2017 baada ya kuingia ukumbini akiwa ndani ya jeneza.

Kwa tamaduni za Kiafrika, inakatazwa mtu kuigiza kifo kwa kile watu wanaamini kwamba kufanya hivyo ni sawa sawa na kukaribisha mauti katika familia au nafsi ya mtu.

Maoni yako ni yapi kuhusu wasanii kutumia njia kama hizo kuwakosha mashabiki?