"Usinipe pole faraghani!" Akothee atoa onyo kali baada ya kufichua mambo hayakuwa sawa kwake

Mwimbaji huyo amewataka watu kuacha kujifanya kumhurumia faraghani kwani alipambana na mambo yake bila kuwashirikisha.

Muhtasari

•Akothee amewaonya watu dhidi ya kumpigia simu ili kupata habari zaidi baada ya kufichua anachopitia.

•Akothee alidokeza kuwa anaendelea vyema na kudokeza kuwa hahitaji kufarijiwa na watu ambao hajuani nao.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji Esther Akoth almaarufu Akothee amewaonya watu dhidi ya kumpigia simu ili kupata habari zaidi baada ya kufichua anachopitia.

Siku ya Jumapili jioni, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alitoa taarifa ya kutia wasiwasi kuhusu yale ambayo amekuwa akipitia katika miezi michache iliyopita akisema kwamba ametoka katika mahali pa hatari sana.

Inaonekana kuna watu wengi walijaribu kuwasiliana naye baada ya taarifa hiyo kwani mwanamuziki huyo sasa amejitokeza kuonya watu dhidi ya kumtafuta huku akisema ni unafiki tu.

"Ni dharau kunipigia simu kulingana na hali yangu. Kwa hakika haupigi simu au kuwasiliana nami kwa sababu unajali. Unapiga simu kwa sababu unataka habari za moja kwa moja. Acha ujinga huo," Akothee alisema kupitia Instagram.

Aliongeza, "Wakati ninachapisha maswala yangu, najua tu kuwa nimepambana nayo nje ya mtandao na haiko kifuani mwangu. Na nisipokupigia simu kwa faragha, usinipe pole faraghani. Baki hapo kwa ukurasa wa shabiki, subiri habari kama kila mtu, wewe sio maalum. Watu wanajifanya ndio sitaki maishani."

Mama huyo wa watoto watano alidokeza kuwa anaendelea vyema na kudokeza kuwa hahitaji kufarijiwa na watu ambao hajuani nao.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Katika taarifa yake Jumapili jioni, Akothee alifichua amekuwa akihudhuria vikao vya ushauri maalum na mtaalamu wa kisaikolojia na kujaribu kupona faraghani kwa miezi miwili iliyopita katika juhudi za kurejesha afya yake ya akili.

Alifichua kuwa matatizo yalianza baada ya kupata ukweli na maelezo fulani ya kutisha ambayo yalimfanya aingiwe na hofu na kumfanya aingie kwenye dimbwi  la mawazo.

"Nimetoka eneo hatari sana na nimekuwa nikipona kwa faragha, niko kwenye mwezi wa pili wa therapy kufuatia kiwewe nilichopitia baada ya kujua ukweli na mambo mabaya ambayo yaliniacha nikitetemeka, Zilipita siku bila chakula. na hakuna kulala, nilihoji na kujijibu mwenyewe, imekuwa nzito sana. Siku zingine, usiku ungekuwa siku na kuniacha mimi nikitazama nje ya dirisha nikikadiria  yasiyokuwepo, ningejipata nikitetemeka kwa sababu ambazo siwezi kuelezea, na kumbuka bado nilikuwa na kazi ya kufanya, familia na ufalme wa kulinda. Bado nililazimika kuweka uso mkali na kuwaburudisha mashabiki wangu,” alisema. 

Aliwashukuru wote waliosimama naye wakati wa nyakati ngumu alizopitia na kumsaidia kutembea katika safari ya uponyaji ikiwa ni pamoja na marafiki wake wa karibu, familia na meneja wake Nelly Oaks ambaye amemtaja kama rafikiye mkubwa.

"Nelly Oaks amekuwa akipiga simu haraka, akinipigia bila kukoma na alikuwa akiogopa simu yangu ilipokatika, watoto wangu kisawa sawa hasa wasichana tulihakikisha tunaweka timer ili kuangalia kama niko sawa. Rue alinifuata Ulaya kwa hofu. ya kunipoteza, mtoto alinikalisha hadi nikasimama kwa miguu yangu,” alisema mwimbaji huyo.

Aliongeza, "Nilianza kwa kufuatilia mienendo yangu, niligundua kuwa nilikuwa nikilemewa na hisia mara kwa mara bila sababu, hata mahojiano rahisi tu. Nilikuwa nimekosa utulivu, na sikuweza kuweka kidole juu yake. Sikuwahi kujua kuhusu Unyanyasaji wa Kihisia, hadi nilipoanza matibabu. Nilikuwa katika hali mbaya ya akili iliyonifanya nilipe ksh 50,000 kwa saa kwa kipindi cha saa moja na mtaalamu wa kwanza. Nilikuwa nikitetemeka na kupoteza nguvu, hamu ya kula, usingizi, hofu na hata kupoteza motisha katika kufanya mambo niliyopenda kufanya.”

Kufuatia hilo, amewaomba watu kuendelea kumuunga mkono na kumuombea yeye na familia yake wakati wakiendelea kurekebisha mambo faraghani.