Msanii anayefanya vizuri katika tasnia ya Bongo Fleva, Marioo kwa mara ya kwanza amepasua mbarika kwa nini hakuwahi kuingilia kati ugomvi na michambo ya kimitandaoni baina na mpenzi wake Paula dhidi ya mpenzi wake wa zamani, Rayvanny na babake wa zamani wa kufikia, Harmonize.
Akizungumza kwa kauli zenye ukali mithili ya simbabukaa aliyejeruhiwa katika kituo cha East African Radio, Marioo alisema kwamba aliyaona maugomvi hayo bali aliamua kukaa kimya lakini akatoa onyo kwa Rayvanny na Harmonize kwamba safari hii wakijaribu kumtibua Paula basi watakiona cha mtema kuni.
Marioo alisema kwa sababu anampenda sana Paula, yuko tayari kumvaa mtu yeyote atakayekanyaga kwenye kumi na nane zake, na kutoa onyo kwamba hatomsaza mtu yeyote awe nani au nani ambaye atajaribu kumchokoza mpenzi wake.
“Mimi sidhani kama shida ya mpenzi wangu na wabaya wake, sawa kwa sasa napendana naye na naweza nikavaa ugomvi wake wowote, lakini binafsi mimi sikutaka iwe hivyo… sasa hivi mtu yeyote yaani, awe nani awe nani, yaani yeyote yule, sasa hivi mchumba wangu keshamalizana na hao watu wote, hana shida na mtu yeyote kaamua kuzingatia tu maisha yake,” Marioo alisema.
“Amegombana sijui na Ex wake wamechambana kishenzi, mimi nimeona nimekausha kwa sababu ilibidi iwe hivyo, hainihusu. Maneno maneno wametupiana huko sijui na aliyekuwa babake wa kufikia nimekausha kwa sababu hayanihusu, mambo yote keshaisha. Sasa hivi mtu yeyote…mtu yeyote akiyatimba sasa hivi, nipo naye, tutaongea na yeye vizuri,” Marioo aliongeza kwa ukali.
Msanii huyo na Paula wamekuwa wakisemekana kuwa kwenye uhusiano ambao pia umetiwa kidole na mamake Puala, Kajala ambaye alifichua kwamba Marioo amekaribishwa nyumbani kupeleka mahari muda wowote.
Marioo siku chache zilizopita alidaiwa kutoa mahari ya milioni 100.