Rose Muhando aubariki wimbo wa Prof Jay akielezea madhira ya siku 462 hospitalini

"Mungu wa Miungu na ni kamanda wa vitu, anatupigania daima watoto wake, pole sana kaka yangu @professorjaytz uliyoyapitia ni ushuhuda wa kukujenga zaidi ki imani" Muhando aliandika.

Muhtasari

• Katika wimbo huo, Professor Jay alihadithia jinsi alianza kujisikia mnyonge baada ya kumaliza ziara ya shoo kadha.

Professor Jay na Rose Muhando
Professor Jay na Rose Muhando
Image: Instagram

Malkia wa miziki ya Injili, Rose Muhando ameubariki wimbo mpya wa rapa Professor Jay – Siku 462 – ambapo anasimulia kwa mapana na marefu jinsi alijipata hospitalini na kuishia kulazwa kwa Zaidi ya mwaka mmoja.

Jay aliachia wimbo huo siku mbili zilizopita akimshirikisha msanii wa injili Walter Chilambo, ukiwa umebeba ujumbe mkubwa wa kurudisha shukrani kwa Mungu kwa kumtoa mashimoni.

Muhando aliguswa na wimbo huo na kuchukua kipande ambacho alikipakia kwenye Instagram yake na kwa niaba ya Jay, akamshukuru Mungu kwa kumrudishia afya yake mpaka amesimama tena na kuweza kuingia studioni kuachia mistari – japo kwa sauti mbovu, aliyosema kwamba ni kutokana na kutobolewa koo na madaktari.

Mungu ni Daktari wa Madaktari, ni Mungu wa Miungu na ni kamanda wa vitu, anatupigania daima watoto wake, pole sana kaka yangu @professorjaytz uliyoyapitia ni ushuhuda wa kukujenga zaidi ki imani, Mungu wetu hashindwi na jambo. Nakuomba wewe Mtanzania, Mkenya au kutoka popote pale, pita kwenye platforms zote kuusikiliza huu wimbo 462 kuna sehemu utakutoa na kukupa tumaini jipya,” Rose Muhando aliandika.

Katika wimbo huo, Professor Jay alihadithia jinsi alianza kujisikia mnyonge baada ya kumaliza ziara ya shoo kadha wa kadha kwenye mikoa mingi ya Tanzania.

“Januari 24, 2022 nilijisikia vibaya na kudhoofika mwili, mke wangu alinikimbiza hospitali ya Kitengule, baada ya huduma ya kwanza wakanikimbiza Lugale, hali ilikuwa mbaya wakanipima upesi upesi, nikakimbizwa Muhimbili kwa ambulensi ya jeshi, nilipofika Muhimbili moja kwa moja ICU, ahsante sana Mungu kila wakati I see you,” sehemu ya mistari kwenye wimbo wa Professor Jay inaimba.

Msanii huyo kama jina la wimbo wake, alifichua kwamba alitrumikia katika kitanda cha hospitali kwa siku 462 bila kujitambua kuwa yeye ni nani.

Ni hivi majuzi tu alifanya mahojiano yake ya kwanza tangu kupata fahamu na kukiri kwamba alitumia gharama ya Zaidi ya shilingi milioni 50 za kitanzania kwa kuchomwa sindano tu, gharama za kuosha figo zikiwa bado hazijahesabiwa.

Kwa sasa, Jay ameanzisha wakfu wake wa kutoa hamasa kuhusu tatizo la kufeli kwa figo na jinsi wathirika wanaweza kupata msaada kwa mapema kabla tatizo hilo halijawa kubwa.