Msanii anayechipukia kwa kazi kwa miziki ya Amapiano kutoka Tanzania, Chino Kid maarufu kama Chino Wanaman ametoa tamko la kihisia siku chache baada ya kupata ajali mbaya ya barabarani akiwa na rafiki zake.
Chino kupitia ukurasa wake wa Instagram, alitoa tamko la kumshukuru Mungu katika tukio hilo la Jumamosi lililosababisha kifo cha mmoja wao ambaye ndiye alikuwa anaendesha gari hilo.
Chino alisema kwamba kwa sasa hawezi sema lolote kwa sasa kwani hajui jinsi kila kitu kilitokea bali ni Mungu tu ana majibu ya ajali hiyo na hata ya kifo cha rafiki yake.
“Asante Mungu wangu kwa kila kitu kwenye maisha yangu wewe ndie ulioniumba wewe pia ndio ulionipandisha wewe ndio ulioniokoa na wewe ndio uliamua kumchukuwa ndugu yangu so majibu ya yote unayo wewe naimani utajibu kwa wakatii sahihi kwa kila kibaya chochote kinachotaka kujaribu kuaribu maisha yangu japokuwa naimani kuwa ni mpango wa mungu tu,” aliandika Chino kwenye aya hiyo ya kutia huruma.
“Haya yote kutokea binafsi siwezi ku dill na chochote kwenye hii dunia au kufikiria lolote lililosababisha kupata hili tatizo na asante kwa kila kitu asante kwa watu wote mnaotuaombea dua,waliotutia moyo na waliotusaidia kwa hali na mali tangu pale mliposikia matatizoo amen,” alimaliza kwa dua.
Siku mbili zilizopita Radiojambo.co.ke tuliripoti kwamba Chino na wenzake walipata ajali mbaya baada ya gari lao kugongana na lori la kusafirisha mafuta.
Katika taarifa yake Jumapili alasiri, Chino ambaye alinusurika kwenye ajali hiyo mbaya ya barabarani iliyohusisha gari lao aina ya Toyota Alphard na lori la mafuta siku ya Jumatatu mchana aliomboleza rafiki yake Nabeel ambaye kwa bahati mbaya alipoteza maisha Jumapili asubuhi.
Katika maelezo yake, mwimbaji huyo wa Bongo Amapiano alifichua kuwa marehemu Nabeel alikuwa akiweka juhudi kubwa katika kazi yake ili kumpa malezi mazuri mtoto wake ambaye sasa amemuacha. Chino hata hivyo ameahidi kuendelea kumtunza mtoto huyo ili kutimiza matakwa ya marehemu.