Mwanasosholaiti Amber Ray ametupa dongo kwa wabaya wake ambao amefichua wengi wao hawakuwa wanamtakia mema katika uhusiano wake na mpenzi wake Kennedy Rapudo.
Siku moja tu baada ya kufichua sura ya mtoto wao – ambaye kwa asilimia kubwa alionekana kuchukua usuli wa baba, Amber Ray amefichua kwamba wengi walikuwa wanasubiri waone akiwa hamfanani babake.
Siku moja iliyopita, Amber Ray na Kennedy Rapudo waliandaa tafrija la kufichua sura ya mwanao Africanah, ikiwa ni miezi minane tangu alipozaliwa.
Amber Ray alisema kwamba wengi walikuwa wanadhani mtoto huyo atamfanana mtu mwingine tofauti na babake ili wapate nafasi ya kumbatiza majina mabaya mabaya ya kishangingi.
Lakini baada ya kufanana babake, Amber Ray amesema wabaya wake sasa wamebaki na tope katika nyuso zao, akisema kwamba ni Mungu amewanyamazisha wale waliokuwa wakisubiria siku hiyo kuona mtoto hamfanani babake ili wamtungie aya za kumuapiza.
“Najua wasionipenda walikuwa wanangoja Africanah Rapudo akose kufanana na babake ndio waniite Mal**a kweli kweli lakini Mungu ni nani?” Amber Ray alisema kwa kujishebedua.
Baada ya kutambulisha sura ya mwanao katika mitandao ya kijamii, mtoto huyo alipata kazi yake ya kwanza kama balozi wa bidhaa za vipodozi akiwa na umri wa miezi 8.
"Anapokua, nashuhudia mageuzi ya roho changa inayopitia safari ya maisha. Yeye si tu binti yetu tu; yeye ndiye rubani mwenza wetu katika tukio hili, akitufundisha masomo mazito ya upendo, uthabiti, na dhamana isiyoweza kuvunjika ambayo inatuunganisha pamoja,” Kennedy Rapudo alisema katika taarifa.
Mwanasosholaiti Amber Ray kwa upande wake alisherehekea binti yake kwa kupata dili nzuri ya matangazo na duka la urembo la watoto.
"Uso rasmi wa @enkwanzi_beauty baby products. Boss baby mwenye umri wa miezi 8. hongera @africanahrapudo," aliandika.