Mwimbaji wa nyimbo za Injili mwenye utata Chris Mosioma, almaarufu Embarambamba, amejitokeza na kuomba msamaha baada ya Bodi ya Filamu na Uainishaji nchini (KFCB) kumuagiza kuzifuta video zote zenye maudhui chafu kwenye chaneli yake ya YouTube kwa kile ambacho shirika hilo lilisema ni maudhui chafu yanayoharibu maadili ya jamii.
Katika video fupi iliyosambazwa kwenye mitandao yake ya kijamii, Embarambamba aliisihi KFCB kutomchukulia hatua, akisema watoto wake watateseka ikiwa maudhui yake yataondolewa kwenye majukwaa ya mtandaoni.
Mwimbaji huyo alisema anategemea tu maudhui yake kwa mapato, ambayo yeye hutumia kulisha familia yake, na hatua ya hivi punde ya KFCB itawatia matesoni.
"Tafadhali naomba msamaha, kwa sababu ile barua mmeniwekea kwa mkono wangu ni nzito. Najua bianadamu aliyezaliwa na mwanamke hawezi kosa kufanya makosa, na huomba msamaha," Embarambamba aliomba.
Pia alitangulia kuomba msamaha kutoka kwa Wakenya, akisema yeyote aliyekerwa na nyimbo na maudhui yake, anapaswa kupata moyoni mwao kumsamehe.
"Mimi nilijua nafanya nyimbo hizi za Mungu watoto wangu wasome, wakule vizuri na mimi nikae vizuri kwa maisha yangu. Lakini Wakenya, sina uwezo," aliongeza.
Embarambamba alikiri zaidi kwamba kile ambacho amekuwa akifanya mtandaoni si sahihi, akisema anatarajia kubadilisha maudhui yake ili kuakisi matarajio ya jamii.
"Mngeniskiza. Kuliko nidelete nyimbo zangu kutoka Youtube, mnibakishie kidogo ili nisomeshe watoto wangu na wapate kitu cha ukubwa. 6.4 million views yote jamani?" Embarambamba alizidi kuomba.
Haya yanajiri baada ya KFCB kumuidhinisha Embarambamba pamoja na msanii mwingine aliyetambulika kama Getombe kutokana na nyimbo zao za injili zenye utata.
KFCB iliamuru kuondolewa kwenye YouTube na mitandao ya kijamii kwa nyimbo zote zilizofanywa na wasanii hao wawili.
Zaidi ya hayo, walizuiwa kufanya nyimbo chafu zaidi kwa jina la muziki wa injili.