Meneja na msanii Stevo Simple Boy, Chingiboy Mstado amefunguka kwamba akaunti za mitandao ya kijamii za Stevo ziko chini ya himaya yake.
Katika mazungumzo na SPM Buzz, Chingiboy Mstado aliweka wazi kwamba akaunti hizo anazo yeye lakini akasema kwamba yuko tayari kuzirudisha kwa msanii huyo baada ya kusitisha uhusiano wake wa kikazi na yeye.
Chingiboy akifunguka sababu zake za kushikilia akaunti hizo licha ya kusitisha uhusiano wa kikazi na msanii huyo wa ‘Freshi barida’, alisema kwamba anataka alipwe kiasi cha pesa alizotumia kuzikomboa akaunti kutoka kwa uongozi wa awali.
“Akaunti zake zilikuwa zimeshikiliwa na uongozi wa awali, mimi nilipiga simu na meneja wa zamani tukazungumza kwa saa 4 akaniambia amenisikiliza na kuomba nimpe ‘kitu’ kidogo ili aachilie akaunti za msanii,” Chingiboy alisema.
“Kitu hapa inamaanisha hela, nilitoa pesa kadhaa. Akaunti sasa ziko na Chingiboy lakini niko tayari kuzirudisha kwake kwa sababu ni zake na zinafaa kumsaidia, mimi niko tayari,” aliongeza.
Hata hivyo, licha ya kuwa tayari kuzirudisha akaunti, Chingiboy alisema kwamba atahitaji kurudishiwa gharama alizotumia kuzikomboa, akisema hatoomba kurudishiwa gharama alizotumia kwa msanii huyo.
“Sitaki niweke mambo ambayo nimemfanyia, mimi nilikuwa namsaidia. Hizo zenye niliwekeza kwake sitaki wanirudishie lakini zile nililipa kwa MIB kupata akaunti, ndio tu nataka nirudishiwe,” Chingiboy alisema.
Kama meneja, Chingiboy alithibitisha kwamba yeye ndiye amekuwa akiongoza kulipa kodi ya kila mwezi ya alikokuwa akiishi Stevo Simple Boy huko Buruburu.
Chingiboy alisema ‘rent’ ya Stevo ilikuwa inatokana na kazi ya usanii lakini kwa uhalisia, yeye kama neneja muda mwingi ndiye alikuwa anatumia hela zake kumlipia Stevo nyumba.
“Mara nyingi rent yake nilikuwa nalipa kwa pesa zangu, kwa sababu hakuwa anapata shoo sana. Pesa zote zilikuwa zinakuja karibia elfu 15 kwa kila mwezi,” Chingiboy alidai.