Mzalishaji wa aina mbalimbali za midundo kwa miziki ya kizazi kipya nchini Tanzania, S2Kizzy ameibuka na kudai kwamba anaidai nchi ya Tanzania deni kubwa na zito la heshima.
Produsa huyo ambaye pia amekuwa akifanya kazi na Diamond, Marioo, Mbosso miongoni mwa wasanii wengine alikuwa anatilia kwenye mizani mjadala ulioanzishwa na Harmonize kuhusu ni wimbo gani bora kwa mwaka 2023.
Harmonize kwa muda mrefu amekuwa akipania kwamba Single Again ndio wimbo bora mwaka jana huku Jux na Diamond pia walishikilia kwamba kolabo yao ya Enjoy ndio wimbo bora.
Produsa S2Kizzy amedai kwamba bila yeye, tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania haingekuwa katika kiwango ambacho ipo kwa sasa.
Produsa huyo alijitapa kwamab ndiye mzalishaji muziki mwenye ubora wa pekee ambaye bado yuko hai na kusema bado Tanzania haijampa maua yake kwa heshima inayostahili.
“Mimi ndiye mzalishaji muziki bora aliye hai. Katika ila fact, sio kwa takwimu, ngoma kali, ngoma kubwa, ngoma maarufu… zote kwa midundo yote. Kwa hiyo kwa asilimia kubwa ya ngoma kali katika nchi hii [Tanzania] zimezalishwa na mimi. Mimi ndiye mkali wao, hii nchi ina deni langu kubwa,” S2Kizzy alisema.
Miezi michache iliyopita, tuliripoti jinsi Diamond alidai kutambua kipaji cha produsa huyo na kuanza kufanya kazi na yeye.
Diamond katika mahojiano, alifichua kwamba alisikia kazi ya S2Kizzy kwenye wimbo wa Mbosso na akaamua kwamba ni mtu mwenye talanta ya aina yake ya kufanya muziki na yeye.
Asilimia kubwa ya nyimbo za Diamond ambazo zimetoka katika kipindi cha kama miaka 3 iliyopita zote zimezalishwa na S2Kizzy.