Ndoto yangu awali ilikuwa kuwa mchezaji na kuipeleka Tanzania Kombe la Dunia - Harmonize

Katika albamu yake ya tano, ‘Muziki wa Mama’ Harmonize aliachia ngoma zote za kumsifia rais Samia Suluhu Hassan, baadhi wakizitaja ngoma hizo kama za kampeni kuelekea uchaguzi wa Tanzania wa mwaka Kesho.

Muhtasari

• Harmonize alisema kwamba ana albamu nyingine kwa jina World Cup ambapo amewashirikisha wasanii kutoka mataifa mbalimbali.

HARMONIZE
HARMONIZE

Msanii Harmonize amefichua kwamba tangu utotoni, ndoto yake haikuwa kuwa mwanamuziki bali kuwa mwanasoka mkubwa wa kuipa nchini yake taswira ya mafanikio kwenye ulingo wa dunia.

Akizungumza na Clouds Media, Harmonize alisema kwamba ndoto yake kabla ya kuingia kwenye muziki ilikuwa ni kuwa mchezaji wa kwanza kuifanikisha Taifa Stara ya Tanzania kufuzu kushiriki mashindano ya kombe la dunia.

Murugenzi huyo wa lebo ya muziki ya Konde Music Worldwide alisema kuwa hata hivyo hilo halikuweza kutimia lakini akasema baada ya kutusua kwenye muziki, lengo limebadilika na sasa anatazamia kuufanya muziki wa Tanzania kujulikana dunia nzima.

Harmonize alifunguka kwamba tayari ana albamu mpya ambayo hata hivyo hakutaja tarehe ya kuiachia, akisema kwamba itamkalia ngumu kwani awali alishawaaminisha mashabiki wake kwamba alikuwa anaacha kabisa masuala ya kuachia albamu na kujikita katika muziki wa ngoma moja baada ya nyingine.

“Mwaka jana, wazo langu lilikuwa ni kuachia albamu tofauti kabisa, kwa sababu nimefanya kolabo tofauti tofauti na wasanii wa Marekani. Kusema kweli ninaweza nikakupa kidokezo cha albamu ambayo nataka niachie baadae…”

“Nitajifikiria kwa sababu nilisema Muziki wa Mama [Albamu yake ya hivi majuzi] ndio ingekuwa albamu yangu ya mwisho lakini sasa bado kuna albamu nyingine inaitwa ‘World Cup’ imekamilika tayari. Ndoto yangu ilikuwa ni kuipeleka Tanzania Mashindano ya kombe la dunia lakini ikashindikana na kwa bahati nzuri nilifanikiwa katika muziki na nilitengeneza albamu ya ‘World Cup’ ambayo ina karibia msanii kutoka kila nchi, ndio maana nikaiita World Cup,” Harmonize alifafanua.

Akirejelea hapo kwa msanii kutoka karibia kila nchi, Harmonize alitaja baadhi ya mataifa ambayo wasanii wake wamo kwenye albamu hiyo yake ambayo itakuwa ya sita katika taluma yake ya muziki tangu kuondoka Wasafi na kujisimamia kivyake.

“Kuna wasanii wa Marekani, Ufaransa, Afrika Magharibi, Afrika Kusini, Jamaika… ndio maana nikaiita World Cup na ndio ilikuwa itoke kwanza lakini nikasema kama kijana mzalendo ngoja kwanza nitenge wakati wa kumzungumzia rais wangu.”

Katika albamu yake ya tano, ‘Muziki wa Mama’ Harmonize aliachia ngoma zote za kumsifia rais Samia Suluhu Hassan, baadhi wakizitaja ngoma hizo kama za kampeni kuelekea uchaguzi wa Tanzania wa mwaka Kesho ambapo Samia anatarajia kuwania awamu nyingine baada ya kuapishwa kama raia mwaka 2021 kufuatia kifo cha aliyekuwa rais, John Pombe Magufuli.

Kipindi hicho, Samia alikuwa naibu wa rais.