Mwanasosholaiti Corazon Kwamboka adokeza kurudi kwenye taaluma ya uwakili

Kwamboka aliangazia matukio ya hivi majuzi katika maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.

Muhtasari

•"Nilipokuwa mdogo, nilikuwa na ndoto ya kuwa wakili wa kutetea wale wasioweza kujitetea wenyewe," alisema Kwamboka.

•"Nia yangu iko wazi na bayana ;kutetea walio kwenye hatari, hasa kina mama wanaohitaji sauti," alitangaza Corazon.

CORAZON KWAMBOKA
Image: HISANI

Corazon Kwamboka, mwanasheria ambaye katika miaka ya hivi karibuni amejikita zaidi katika kuunda maudhui badala ya kufanya kazi kama wakili wa Mahakama Kuu, ametangaza mabadiliko makubwa katika maisha yake.

Akizungumza kwenye Instagram, Kwamboka aliangazia matukio ya hivi majuzi katika maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.

"Nilipokuwa mdogo, nilikuwa na ndoto ya kuwa wakili wa kutetea wale wasioweza kujitetea wenyewe," alishiriki ujumbe Kwamboka.

"Licha ya kwamba njia yangu ilinipeleka sehemu nyingine kwa wakati huo, hamu ya kufanya mambo kwa utofauti ilibaki.

Kusoma sheria kwangu kulihamasishwa na waandishi kama John Grisham, haikuwa tu ndoto yangu pekee bali pia ya wazazi wangu," aliendelea Kwamboka.

Akiendeleza cheti chake cha kufanya kazi kama wakili, Corazon alitafakari safari yake baada ya shule ya sheria, akijihisi hana uhakika jinsi ya kutumia shahada yake kwa makuzi na ufanisi.

"Nilitafuta mwongozo kupitia sala, nikiomba ishara ya kuniongoza kutumia ujuzi wangu kwa kuhudumia wengine," alieleza Kwamboka

"Hivi karibuni, katika wito wa haki baada ya vifo vya waandamanaji, nilihisi wajibu wa kurudi kwenye sheria."

"Nia yangu iko wazi na bayana ;kutetea walio kwenye hatari, hasa kina mama wanaohitaji sauti," alitangaza Corazon.

"Misheni hii mpya inachochea roho yangu. Na cheti changu cha kufanya kazi kimeboreshwa, nipo tayari kuwatetea kwa moyo wangu wote wale wanaohitaji msaada zaidi."