Rapa ambaye pia ni mkuza maudhui kupitia jukwaa la YouTube, Diana Marua ameandikisha historia kwa kuwa Mkenya wa kwanza wa kike kutambuliwa na YouTube kwa kufikisha wafuasi milioni moja na Zaidi.
Diana Marua mapema Jumatatu alipokezwa Golden Button kutoka YouTube kama utambulisho kwa hatua hiyo ya kipekee.
Akieleza furaha yake, mkewe Bahati alihadithia jinsi alipata wazo la kuanzisha chaneli ya YouTube miaka si mingi iliyopita bila kujua kwamba ndio ulikuwa mwanzo wa safari yake yenye mafanikio makubwa.
“Msanii wa Kwanza wa Kike na Muundaji Maudhui nchini Kenya Kupokea Kitufe cha Dhahabu cha YouTube kwa kufikia Wasajili Milioni 1 😭🙏”
Maneno yanashindwa kueleza shukrani zangu kwa kila mtu ambaye anatazama maudhui yangu. Nilianza Uundaji wa Maudhui ili Kuhamasisha, Kuelimisha na Kuunganishwa na watu wangu kote Ulimwenguni. #DIANABAHATI sio tu chaneli ya youtube, ni NGUVU,” alisema.
Aidha, mama huyo wa watoto watatu alisema kwamba alianzisha chaneli hiyo mwaka 2019 na kuanza kukuza maudhui kwa kujiamini wakati wa janga la covid-19 mnamo 2020.
“Nilifungua chanel hii Julai 2019, nikawa makini na kuunda maudhui mwaka wa 2020 (Wakati wa Covid). Nikafikisha subscribers Milioni 1 tarehe 17 Februari 2024. Imechukua miaka 5 ya kufanya kazi kwa bidii, kujitolea na uthabiti. Imechukua Taifa Nzima kufika hapa. Kwa kila mtu anayetazama na kuunga mkono maudhui yetu, Kitufe hiki cha Dhahabu ndicho USHINDI wetu!” alisema kwa furaha.
Mrembo huyo ambaye hivi majuzi walizindua kipindi chao cha uhalisia kwenye jukwaa la Netflix na mumewe alishukuru kila mtu ambaye ametoa mchango katika safari yake kuelekea wafuasi milioni moja, bila kusahau juhudi za mumewe ambaye amekuwa akimpa shavu nyakati zote.
“Familia bado inakua na ninachoweza kusema ni kwamba, ninathamini kila mmoja wenu. Dee Nation, Mungu Awabariki Wote. Kitufe cha Dhahabu kiko nyumbani. Kwa Hubby wangu @BahatiKenya umekuwa Mfumo wangu Mkubwa wa Usaidizi na Kiongozi wangu wa Kushangilia. Asante kwa kunishika mkono katika safari hii. Nakupenda ❤️🙏❤️”