“Omtatah, Nameless, Boniface Mwangi na wengine katika Shujaaz concert sio Gen Z” – Robert Alai

“Kwa kweli, ninaona kundi la akina Methusela wenye nia ya kibiashara wakitumia itikadi ya Gen Z. Sioni Gen Z katika orodha hii. Halafu usanidi huo haungeweza kugharimu chini ya Ksh 5 milioni. Nani alifadhili hiyo?” alihoji Zaidi.

Muhtasari

• MCA huyo alikwenda mbele na kudai kwamba anachokiona kutoka kwa majina aliyotaja ni kundi la watu wenye lengo la kujificha ndani ya vijana wa Gen Z ili kufanikisha malengo na maslahi yao.

ROBERT ALAI, MCA KILELESHWA.
ROBERT ALAI, MCA KILELESHWA.
Image: FACEBOOK

Mwakilishi wadi wa Kileleshwa, Robert Alai ameibua madai akisema watu wote ambao walikuwa katika mstari wa mbele kuongoza tamasha la kuwakumbuka walioangamia kwenye maandamano ya kupinga mswada wa fedha sio kutoka kizazi cha Z.

Kupitia kurasa zake kwenye mitandao ya kijamii, MCA huyo wa chama cha ODM alisema kwamba alifuatilia tamasha hilo kwa umakini na watumbuizaji wote pamoja pia na waliozungumza ni watu Zaidi ya miaka 35.

Jumapili, vijana walifurika katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi katika tamasha la Shujaaz ambapo lengo lilikuwa kuwasha mishumaa kwa ajili ya kumbukumbu ya waliofariki wakati wa makabiliano na polisi maeneo mbali mbali nchini.

Hata hivyo, Alai alidai kwamba wote waliohusika katika kupanga tamasha hilo ni watu nje ya mabano ya Gen Z akiwataja baadhi yao na kuuliza kama kweli wanastahiki kuwekwa kwenye kategoria ya Gen Z.

“Ngoja niulize swali lisilo na hatia. Katika Tamasha la Mashujaa Memorial, hawa walikuwa wazungumzaji au wasanii; Nameless, Bien, Juliani, Maji Maji, Khaligraph Jones, Okiya Omtatah, Boniface Mwangi…Nani kutoka hapo anatoka Generation Z? Hakuna aliye chini ya miaka 40 kati ya hao hapo,” Alai alihoji.

MCA huyo alikwenda mbele na kudai kwamba anachokiona kutoka kwa majina aliyotaja ni kundi la watu wenye lengo la kujificha ndani ya vijana wa Gen Z ili kufanikisha malengo na maslahi yao.

Pia alihoji chanzo cha hela zilizotumika kupanga hafla hiyo, akisema vyombo vilivyotumika haviwezi kuwa chini ya shilingi milioi tano kwa kukodisha kwa siku moja na kudai kwamba vijana hao hawangekuwa na uwezo kama huo.

“Kwa kweli, ninaona kundi la akina Methusela wenye nia ya kibiashara wakitumia itikadi ya Gen Z. Sioni Gen Z katika orodha hii. Halafu usanidi huo haungeweza kugharimu chini ya Ksh 5 milioni. Nani alifadhili hiyo?” alihoji Zaidi.