Msanii kutoka Kanada, Drake si mgeni katika suala la kucheza Kamari katika michezo mbalimbali, iwe ndondi, tenisi na hata kandanda.
Katika michuano inayoendelea ya Copa America, Drake alitupa ndoana yake kwenye Kamari akijaribu bahati kwa kuibashiria timu yake ya nyumbani, Kanada kuwashinda mabingwa watetezi Argentina kwenye nusu fainali.
Drake aliwekeza kitita cha dola elfu 300, sawa na shilingi milioni 38.29 pesa za Kenya akitumai Kanada wangeipiga Argentina yake Messi kwenye nusu fainali hiyo.
Hata hivyo, matokeo yalikuwa kinyume chake kwani Kanada ilibanduliwa kwenye nusu fainali na Argentina kwa kipigo cha mabao 2-1
Rapa huyo angeshinda kitita cha dola milioni 2.88, sawa na shilingi za Kenya milioni 368 ikiwa Canada ingefanikiwa kuipiga Argentina.
Chapisho la Drake kuhusu dau hilo ni pamoja na nukuu iliyosema, "Hili linaweza kumpata Messi" akiwa na emoji ya bendera ya Kanada.
Mbio za Canada hadi nusu fainali zilikuwa mshangao mzuri katika mashindano hayo. Kikosi cha kocha mkuu Jesse Marsch kiliingia Copa América nafasi ya 11 kati ya timu 16 kulingana na viwango vya FIFA.
Hii ni mara ya kwanza kwa Kanada kuonekana kwenye Copa America. Timu ya taifa ya wanaume ilikuwa inatafuta taji lake la kwanza katika mchuano mkubwa tangu Kombe la Mataifa ya Amerika Kaskazini mnamo 1990.
Mechi ya Jumanne ilikuwa ni mechi ya pili ya ana kwa ana na Argentina katika Copa America. Canada ilipoteza 2-0 katika mchezo wa kwanza wa kundi la timu zote mbili mnamo Juni 20.
Huo ulikuwa mkutano wa pili kuwahi kati ya nchi hizo mbili. Ya kwanza ilikuwa mechi ya kirafiki ya 2010 ambayo Argentina ilishinda 5-0.