Pasta Ng’ang’a kwa mara nyingine ametetea msimamo wake wa kuunga mkono maandamano ya vijana wa Gen Z yanayolenga kuiwajibisha serikali.
Akizungumza kwenye mkutano wa injili mjini Kitengela, Ng’ang’a alisema kwamba anaendelea kuwaunga mkono kwa sababu wamechukua jukumu la kuwazungumzia wazee yale ambayo hawangesikilizwa.
Hata hivyo, mchungaji huyo alisema kwamba hajazungumzia serikali kwa njia yoyote bali vijana wanamzungumzia.
Kwa utani, Ng’ang’a alisema kwamba hata kama alizungumzia serikali na mtu ampeleke mahakamani akimtuhumu kwa kuizungumzia vibaya serikali, atasingizia umri wake na kumuambia hakimu kwamba huenda alizungumza wakati shinikizo la damu lilikuwa limeongezeka.
“Mimi niko pamoja na Gen Z, niko hapo. Ni vile walisema eti nisiende kwenye maandamano yao eti nitapigwa na kitoza machozi nife. [akicheka] Lakini enyewe safari hii mumetupasha tohara mara ya pili. Hatuongei sisi wazee, tuko na Panadol kwa mfuko,” alisema.
“Sijui hiyo ndio mtu alisema eti mimi nimeongea mambo ya serikali, mimi sijaongea mambo ya serikali, usiniletee wazimu wako. Mimi niko na umri wa miaka 71, hata ukinipeleka mahakamani nitaambia hakimu presha ilikuwa juu. Niko na miaka 71 na presha ya wazee huwa wakati mwingine yale maneno anazungumza hayajui,” aliongeza huku akicheka.
Wiki jana baada ya rais Ruto kulivunja baraza lake la mawaziri, Ng’ang’a katika video iliyoenezwa mitandaoni alionekana akicheka na kumpongeza rais kwa kuwafukuza wote aliowataja kuwa wabadhilifu.
Mchungaji huyo amekuwa na mzozo wa ardhi linakokaa kanisa lake, baada ya kutaarifiwa mapema mwaka huu kwamba ardhi hiyo ni mali ya shirika la reli nchini na yeye akisema ardhi hiyo aliulizwa na serikali zaidi ya miaka 20 iliyopita.