“Usinizoee, mimi si pasta wala askofu, mimi ni wa kivita” – Pasta Ng’ang’a aonya wanaomkejeli

“Mimi naitwa James Maina Ng’ang’a, nimepitia vita vyote, hata watu wa magazeti, watu wa habari wananiita eti ooh pasta Ng’ang’a, mchungaji mwenye utata…pumbavu! Redio zote, magazeti yote, watapigana na mimi na hawataniweza.”

Muhtasari

• Mchungaji huyo pia alitumia fursa hiyo kumega ushauri kwa wale ambao wameinuliwa na Mungu na wale wanaotarajia kuwa wachungaji, akiwataka kuacha mchezo katika neno la Mungu.

Mchungaji Ng'ang'a atoa neno kwa wanaokosoa matamshi yake.
Mchungaji Ng'ang'a atoa neno kwa wanaokosoa matamshi yake.
Image: Screengrab//Sasa TV

Mchungaji wa kanisa la Neno Evangelism, James Maina Ng’ang’a ametoa onyo kwa wale wanaomkejeli kwenye vyombo vya habari na mitandaoni wakimtaja kama mchungaji tata.

Akihubiri katika siku ya pili ya kongamano lake la mahubiri mjini Kitengela kaunti ya Kajiado wikendi iliyopita, Ng’ang’a alionya wanaomtaja kama pasta mwenye utata akisema kwamba yeye ni wa kivita zaidi kuliko kuwa pasta au askofu.

“Mimi naitwa James Maina Ng’ang’a, nimepitia vita vyote, hata watu wa magazeti, watu wa habari wananiita eti ooh pasta Ng’ang’a, mchungaji mwenye utata…pumbavu! Redio zote, magazeti yote, watapigana na mimi na hawataniweza.”

“Huyu Mungu wetu si muoga, ni Mungu wa vita, sasa usinizoee, mimi si pasta, mimi si askofu; mimi ni wa kivita. Ukinitafuta utanipata, na ukitaka Amani utapata Amani,” Ng’ang’a alisema kwa onyo.

Mchungaji huyo pia alitumia fursa hiyo kumega ushauri kwa wale ambao wameinuliwa na Mungu na wale wanaotarajia kuwa wachungaji, akiwataka kuacha mchezo katika neno la Mungu.

“Wale mumeinuliwa na Mungu, na wale mnataka kuja kuwa wachungaji, wacheni mchezo, huyu Mungu si kiwete, eti mpigie wanasiasa magoti, ni nini? Wakikucheka wachana nao, usipate kiwewe,” mchungaji huyo aliongeza.

Kwa muda mrefu, Ng'ang'a amekuwa akigonga vichwa vya habari haswa za burudani kutokana na visa vinavyorekodiwa kutoka kwa mahubiri yake.