Mwanablogu wa YouTube Nicholas Kioko amevunja kimya chake kuhusu ya kile alichokitaja kama uvumi na tetesi kwamba amehamisha familia yake kwenda nchini Uingereza.
Akiweka wazi kupitia insta story yake, baba huyo wa mapacha alikanusha uvumi huo lakini akaashiria kwamba huenda hilo likawa moja ya malengo yake siku si nyingi kutoka sasa.
Kioko alisema kwamba japo uvumi huo si wa kuaminiwa, lakini ni kweli kwamba tayari yeye na mkewe Wambo Ashley na wanao mapacha, wamejihami na visa zao za usafiri lakini bado hawajafanya uamuzi.
“Habari zenu kila mmoja, nimesiia tetesi kwamba familia yangu imehamia Uingereza. Licha ya kuwa tayari na Visa zetu, bado hatujafanya uamuzi wowote. Nilikuwa tu nataka kuweka bayana ukweli ili mpate kusikia moja kwa moja kutoka kwangu. Ahsante kwa kuwa waelewa,” Kioko aliandika.
Ikiwa tetesi hizo zitakuwa za kweli, basi Kioko atakuwa anajiunga kwenye orodha ndefu ya watu maarufu wa Kenya ambao walihamia ughaibuni kwa ajili ya kutafuta maisha mazuri.
Wengine ambao tayari wameshaondoka Kenya muda mrefu tu ni pamoja na YouTuber Vincent Mboya, msanii wa genge Nonini Mgenge, Wendy Kimani, Benachi, Shorn Arwa, Willy Paul ambaye hivi majuzi ametangaza kuhamia Ujerumani miongoni mwa wengine.