Jalang’o afunguka kuhangaika kutafuta kura licha ya kuwa na wafuasi wengi Instagram na Facebook

“Kama naweza sema, kama uko na kazi au biashara nzuri ambayo inakupa pesa nzuri na uko na Amani ya nafsi, hauna haja ya kuingia kwenye siasa kwa sababu unaeza hata jipata umeingie kwenye shimo la hasara."

Muhtasari

• "Niligundua mitandao ya kijamii na mazingira ya kiuhalisia ya huku nje ni Nyanja mbili tofauti. Mimi ninaweza kukuambia hivyo,” mbunge huyo wa ODM aliungama.

 

Mbunfe Jalang'o asema hajutii kuutana na rais
Mbunfe Jalang'o asema hajutii kuutana na rais
Image: Instagram

Phelix Odiwuor maarufu kama Jalang’o, mbunge wa sasa wa Lang’ata amezungumzia utofauti mkubwa uliopo baina ya kuwa maarufu kwenye mitandao ya kijamii na kuwa maarufu kwa wapiga kura mitaani.

Jalang’o ambaye mpaka anaingia kwenye siasa alikuwa mmoja kati ya watangazaji maarufu zaidi humu nchini alisema kwamba alikuwa anafikiria umaarufu wake kwenye mitandao ya kijamii ungeoana na umaarufu mitaani wakati wa kupiga kampeni kutafuta kura.

Kwa mshangao wake, Jalang’o alisema kwamba alipitia wakati mgumu kuwashawishi hata watu 30k kumpigia kura licha ya kuwa na ufuasi wa mamilioni ya watu kwenye kurasa zake mitandaoni.

“Uwanja wa siasa ni tofauti sana. Kule mnapambana mpaka kupita michujo yote na kujua kwamba huyu ndiye mtu tunataka, ni uwanja mwingine tofauti. Ni kitu ambacho hata mimi mwenyewe sikuwa tayari nacho.”

“Wakati nilikuwa naingia kwenye siasa, nilikuwa na zaidi ya 2m followers Instagram, 4m followers Facebook lakini nilikuwa nahangaika kupata hata watu 30k kunipigia kura. Niligundua mitandao ya kijamii na mazingira ya kiuhalisia ya huku nje ni Nyanja mbili tofauti. Mimi ninaweza kukuambia hivyo,” mbunge huyo wa ODM aliungama.

Mbunge huyo alitengua dhana kwamba siasa ndio taaluma ya mtu kupata utajiri kwa haraka akisema kuwa siasa ni kitu ghali ambacho mtu usipokuwa makini utapoteza pesa nyingi na kuishia kwenye msongo wa mawazo.

“Watu huku nje wanaona siasa kama njia ya haraka ya kupata pesa nyingi, lakini naweza kuambia kwamba pia inaweza geuka na kuwa njia ghali ambayo utajihusisha nayo.”

“Kama naweza sema, kama uko na kazi au biashara nzuri ambayo inakupa pesa nzuri na uko na Amani ya nafsi, hauna haja ya kuingia kwenye siasa kwa sababu unaeza hata jipata umeingie kwenye shimo la hasara kuliko hata ulivyokuwa umetarajia,” aliongeza.