Msanii na mjasiriamali KRG the Don kwa mara nyingine tena ameonyesha kutofurahishwa na mienendo ya vijana wa Gen Z ambao wamekuwa wakishiriki katika maandamano na kusababisha kuhitilafiwa kwa shughuli nyingi za kila siku za watu wengine.
Kupitia instastory yake, KRG amesema vijana hao wengi wanaona fahari katika kuvuruga shughuli za watu wanaohangaikia mkate wao wa kila siku kwa kisingizio kwamba wanataka kumshauri rais Ruto kuhusu chenye anastahili kufanya.
Alidai kwamba wengi wa vijana hao wanataka kumshauri mtu [Ruto] ambaye amekuwa kwenye serikali tangu akiwa na umri wa miaka 30s hali ya kuwa wengi wao hata huenda hawajui wanakoishi wazazi wao.
“Vuguvugu la Gen Z linadhani kuendesha serikali ni sawa na kuendesha kioski. Wengi wao hata hawajui wanakoishi kina baba zao na wako hapa wanataka kumshauri mtu ambaye amekuwa kwenye serikali tangu akiwa na umri wa miaka 30s. Watu wangu mnastahili kushika adabu zenu na mjue kwamba kuna watu ambao wanafanya biashara jijini na viunga vyake,” KRG aliwazomea.
Msanii huyo alisema kwamba kuna watu wengine ambao nia yao ni kuendesha biashara zao katika mazingira tulivu bila kujali ni nani anafanya nini wapi, na hivyo kuwataka vijana hao kusitisha maandamano yao.
Aliwataka wale wanaodhani kwamba wamekomaa kuendesha serikali kusubiri hadi uchaguzi wa 2027 ili kuchaguliwa.
“Kuna watu ambao hawajali nani anafanya nini. Wanataka tu kufanya biashara kwa sababu wana madeni na bili za kulipa. Kama unadhani unaweza endesha serikali, subiri hadi 2027 na usisahau kuwania. Kuwaheshimu watu ambao wamekuziki kiumri ni jambo muhimu wakati mwingine, hata kama wameenda kombo, tafuta njia ya kuwarekebisha kwa sababu vita na matusi haviwezi kutupa suluhu kama taifa,” msanii huyo aliandika.